SAFARI ya duniani ya nyota wa sinema za Tanzania, Steven Charles Kanumba iliyofikia kilele usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu inaingia hatua muhimu leo kwa marehemu huyo kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu kwa chanzo kinachodaiwa kuwa ni ugomvi baina yake na mpenzi wake wa siri, msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anashikiliwa na maafande wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini Dar.
Habari zinasema kuwa kabla ya safari ya kwenda makaburini, mwili wa marehemu utaagwa katika Viwanja vya Leaders Club, jijini Dar mahali ambapo Kanumba enzi za uhai wake, alipendelea kufika kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wasanii wenzake.
Habari zinasema mbali na kubadilishana mawazo na wenzake, pia alitumia viwanja hivyo kufanyia mazoezi ya viungo.
UTATA WAIBUKA KUHUSU MAHALI PA KUZIKWA
Wakati maandalizi ya maziko ya msanii huyo yalipokuwa yakiendelea nyumbani kwake, maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza Kijiweni, Dar kulikuwa na minong’ono kuwa, familia mbili, kiumeni na kikeni zilivutana kuhusu mahali atakapozikwa marehemu huyo.
Habari zinasema mama wa marehemu aliyewasili Jumapili akitokea Bukoba, Kagera alitaka mwanaye huyo kipenzi akazikwe mjini Bukoba ambako ndiko kwenye asili yake huku ndugu wa baba wakishikilia msimamo kuwa mazishi yawe Shinyanga ambako kuna ukoo wa Kanumba.
KAULI YA KANUMBA
Awali ilidaiwa kuwa wakati wa uhai wake, Kanumba aliwahi kutoa tamko kuwa siku akifa mazishi yake yawe Shinyanga, tena pembeni ya kaburi la babu yake, Mzee Kusekwa Kanumba.
Kwa mujibu wa ndugu mmoja, marehemu aliwahi kusema kuwa katika vitu ambavyo asingependa vitokee ni mwili wake kuzikwa nje ya matakwa yake hayo kwani licha ya kwamba atakuwa amekufa lakini kiroho ataliona hilo.
“Marehemu aliwahi kusema anataka akifa akazikwe Shinyanga, tena pembeni ya kaburi la marehemu babu yake.
“Na akasema kuwa mtu atakayetengua uamuzi huo kwa kumzika eneo hilo lakini si pembeni ya kaburi la babu yake atakuwa amefanya kosa kubwa sana na atamwona kiroho,” alisema ndugu huyo akimkariri marehemu.
TAMKO LA MAMA MZAZI
Jumapili, Aprili 2012, mama mzazi wa marehemu alitoa tamko kuwa amekubali mwanaye azikwe kwenye Makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mama huyo alitoa tamko hilo ikiwa ni majibu ya maombi kutoka ujumbe wa wasanii wa filamu nchini, sanjari na mashabiki wa marehemu na wadau wa filamu ambao walimuomba aamue mwili wa mwanaye uhifadhiwe jijini Dar ili iwe rahisi kwenda kutembelea kaburi lake kama kumbukumbu kutokana na umaarufu wake.
Awali, Jumamosi wasanii wa filamu Bongo walisema wanamsubiri mama wa marehemu wampe ombi hilo kufuatia habari kuwa mwili wa Kanumba ungesafirishwa kwenda Bukoba au Shinyanga kwa mazishi.
MAISHA YA SIKU SABA KABLA YA KIFO
Habari zilizopatikana kutoka kwa watu wa karibu na marehemu zinatafsiri maisha ya siku saba kabla ya kifo chake.
Msanii mwenzake, Emanuel Myamba ‘Pastor Myamba’ alisema Jumamosi kuwa, siku tatu kabla ya kifo, marehemu alimpigia simu akimtaka amwombee sana kwa Mungu bila kumfafanulia mwegemeo wa maombi yenyewe.
“Mimi juzi tu hapa, alinipigia simu akasema Pastor Myamba naomba uniombee sana kwa Mungu, lakini hakuniambia kwa nini ametoa kauli hiyo,” alisema Myamba.
Msanii mwingine wa sinema za Bongo, Jacqueline Wolper alisema kuwa wiki moja kabla ya kifo, marehemu alimwambia kuwa anaamini filamu inayohaririwa (ambayo ni ya Kanumba) iitwayo Ndoa Yangu itazifunika nyingine zote.
“Alisema filamu ya Ndoa Yangu ni bomba, itafunika zote na alitaka itoke baada ya Pasaka, lakini ndiyo hivyo tena,” alisema Wolper huku akidondosha machozi.
Habari zinasema kwenye blog yake (marehemu Kanumba) kazi ya mwisho aliyokuwa akiifanyia matangazo kwa kuweka na picha ni filamu hiyo.
MAISHA YA SIKU SABA BAADA YA KIFO
Akizungumza na paparazi wetu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mh. Zitto Kabwe alisema, marehemu alimuomba ampe mwongozo wa jinsi ya kuanza maandalizi ya kisiasa ili mwaka 2015 ajitose kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini.
Akasema alishamuandalia mwongozo ambao ungemsaidia marehemu kufikia ndoto zake mwaka 2015 na kwamba, ilikuwa wakutane wiki ijayo kwa ajili ya kumkabidhi mwongozo huo.
Katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa mwanamuziki wa Kizazi Kipya, Ambwene Yesaya ‘AY’, kuna mabaki ya meseji ya marehemu Kanumba ambapo walikuwa wakizungumzia safari ya Marekani kwenye Miji ya Las Vegas na San Francisco.
Kanumba: Aa mzee wa Las Vegas.
AY: Tena nimeimisi sana Las Vegas.
Kanumba: Mimi nategemea kwenda huko siku chache zijazo, nitaanzia San Francisco, baadaye Las Vegas.
AY: Basi ukitaka kwenda niambie ili nikuelekeze maeneo ya kula bata.
DAKIKA 45 ZA KIFO
Habari zisizo na chenga zinasema kuwa dakika arobaini na tano kabla ya kifo chake, marehemu na Lulu walifanya mambo ambayo yanaweza kutafsiriwa kwamba mauti yalishamzunguka msanii huyo.
Kwa mujibu wa majirani, ndani ya kipindi hicho, marehemu na Lulu walishatoka nje wakiwa hawapo katika maelewano kiasi cha kuwafanya wapita njia kuwashangaa kutokana na mzozo uliokuwa unaendelea.
Katika tukio hilo, kwa mujibu wa majirani, Kanumba ambaye alikuwa msiri wa mambo yake, hakuonesha kujali watazamaji.
Purukushani hizo zilitawala kwa muda huo na ulipotokea utulivu zikaibuka habari za kuanguka kwa marehemu chumbani kwake, kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako daktari alithibitisha kwamba alishafariki dunia.
KIKWETE ASHINDWA KUKAA IKULU
Katika kuonesha ni jinsi gani kifo cha Kanumba kimewagusa Watanzania, Jumapili ya Pasaka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitinga Sinza kwenye msiba na kuombeleza na mamia ya watu.
Kabla hajaingia kwa wafiwa na kuwapa pole, JK aliitumia nafasi ya kufika eneo hilo kwa ‘kuwapolesha’ waombolezaji wote, hata wale waliokuwa wamesimama nje.
BABA KANUMBA HAPOKEI SIMU?
Ni swali alilojiuliza mmoja wa waandishi wa gazeti hili kufuatia kitendo cha kumpigia simu baba mzazi wa marehemu, Mzee Charles Kusekwa Kanumba siku ya Jumamosi na Jumapili lakini hakupokea.
Hakuna hukumu juu ya kitendo cha mzee huyo kutopokea simu kwani kutokana na uzito wa msiba, inawezekana hawezi kufanya lolote zaidi ya majonzi.
KIMYA MILELE
The Great Steven Charles Kusekwa Kanumba amezimika milele. Hakuna namna ambayo itamfanya aonekane tena katika maisha ya duniani.
Amekwenda na ndoto zake, amekwenda na mipango yake. Ndiye msanii aliyeweza kupenya ukuta mkubwa wa filamu ulioiziba Tanzania isijulikane nje ya nchi kwa kwenda kufanya sinema nchini Nigeria na masupastaa wa huko kama Ramsey Noah na Mercy Johnson.
Marehemu Kanumba aliifanya Tanzania ijulikane nje ya nchi kupitia kazi yake ya sanaa tofauti na ilivyokuwa zamani.
DIAMOND ANASHUHUDIA
Katika kuthibitisha kuwa marehemu aliisaidia vyema Tanzania ijulikane kimataifa, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’, Jumapili iliyopita alitoa ushuhuda jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio, Diamond alisema kuwa kila alipokuwa katika ziara nje ya Tanzania, wengi walikuwa wakimuuliza kama na yeye anatoka Tanzania anakotoka mcheza filamu Steven Kanumba.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina.
Imeandikwa na Shakoor Jongo, Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
No comments:
Post a Comment