Monday, April 30, 2012

Simba Noumaaa


SIMBA jana ilifanikiwa kunyoosha njia yake kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa Al Ahli Shandi mabao 3- 0.

Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ilionekana kulegea kipindi cha kwanza lakini ikarejea cha pili ikiwa na kasi ya hali ya juu.

Wasudani hao ndiyo waliowahi kuanza mashambulizi kwenye mchezo huo katika dakika ya 20 pale Fareed Mohamed alipopiga shuti kali nje ya eneo hatari lakini likatolewa na mlinda mlango Juma Kaseja na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.

Al Ahli Shandi ambayo ilikuwa ikishangiliwa na wale waliodaiwa kuwa ni mashabiki wa Yanga, waliwashangaza watu kwa mchezo wao wa kutotaka kuingia sana ndani ya eneo hatari, kwani walikuwa wakipiga mshuti nje ya eneo hilo kila mara walipokuwa wakishambulia.

Shangwe zilirindima kwenye Uwanja wa Taifa baada ya Simba kupata penalti katika dakika ya 38 lakini kiungo Patrick Mafisango aliunyamazisha uwanja baada ya kupigamkwaju dhaifu iliodakwa na mlinda mlango, Abdelrahiman Ali.

Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu. Simba walianza kuandika bao katika dakika ya 66 kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye kama kawaida yake akifunga bao huwa hashangilii.

Boban alifunga bao hilo akipokea pasi ya Felix Sunzu aliyempinga chenga beki wa Al Ahli na kutoa krosi iliyodakwa na kiungo huyo aliyeutumbukiza mpira kimiani kwa ufundi mkubwa.

Dakika ya 77, Mafisango alisawazisha makosa ya kukosa mkwaju wa penalti baada ya kufunga bao safi akipokea krosi ya Okwi aliyewatoka walinzi wa timu pinzani kabla ya kumtengenezea pasi kiungo huyo raia wa Rwanda. Bao hilo lilisababisha mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga kuanza kutoka uwanjani hapo.

Simba waliweza kuweka mazingira mazuri zaidi ya kucheza hatua ya mchujo baada ya Okwi kufunga bao la tatu katika dakika ya 88 akiunganisha pasi ya Mafisango.

Hadi mwisho wa mchezo matokeo yalikuwa ni 3-0. Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na ameahidi watalinda zaidi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kati ya Mei 11, 12 na 13 nchini Sudan.
“Tunakwenda kutafuta bao moja tu la ugenini na kujitahidi kulinda lango,” alisema Milovan huku kocha wa wapinzani wao, akigoma kuongea.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, aliyekuwa mgeni rasmi wa pambano hilo, Fredrick Sumaye, amesisitiza kuwa, Simba inabidi iandaliwe vizuri kabla ya kucheza mchezo wa marudiano na kwamba hawana sababu ya kushindwa kutwaa kombe hilo kwani wameonyesha wanaweza.

Wakati huohuo, mwenyekiti wa timu hiyo, Ismail Aden Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini, ameiomba serikali iisaidie timu yake kwani hatua waliyofikia ni nzuri na wanaiwakilisha nchini katika michuano hiyo mikubwa ya kimataifa.


Na Wilbert Molandi, GPL

No comments:

Post a Comment