WAKATI Yanga ikijiandaa kuivaa Toto African katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kocha wa Yanga, Kosta Papic, amesaliwa na siku 11 kuendelea kuwa mwajiriwa wa klabu hiyo.
Papic ambaye alibaki Dar wakati kikosi chake kilipoondoka kwenda Mwanza kwa kile kinachodaiwa kuwa anaumwa, amesema kuwa mkataba wake unatarajiwa kufikia tamati Aprili 24, mwaka huu na hakuna mazungumzo yoyote ya kuongezwa kwa mkataba yaliyofanyika mpaka sasa.
“Kuhusu kuwa nje ya klabu kwa sasa ni kwa kuwa naumwa, kuhusu mkataba siwezi kukataa au kukubali lakini ninachoweza kukwambia ni kwamba, mkataba wangu na Yanga unafikia kikomo Aprili 24 na hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamefanyika baina yangu na viongozi wa timu.
“Endapo hali ikiendelea hivi mpaka siku ya mwisho ya mkataba, nitarudi nyumbani nikaendelee na mambo yangu binafsi,” alisema Papic.
Papic alikosekana katika mazoezi ya siku mbili za mwisho ya timu hiyo huku taarifa zikidai kocha huyo amechukizwa na hali ya uongozi kushindwa kujadiliana naye kuhusu mkataba mpya.
Papic ambaye alisema atajiunga na kikosi cha timu hiyo muda wowote endapo atapata nafuu, alisema: “Sijasafiri na timu, nipo hapa Dar, naumwa tumbo lakini majukumu yote ya timu nimemuelekeza msaidizi wangu (Fred Felix Minziro) ambaye yupo na timu, ikiwezekana kesho (jana) kama nitapata nafuu nitaangalia uwezekano wa kuungana nao huko.”
GPL
No comments:
Post a Comment