Friday, March 16, 2012

Ukivunja kiti Taifa, faini milioni 10


WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa litatakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni 10 iwapo kutatokea uharibifu wowote kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia sasa.

Awali, mashabiki wanaodhaniwa wa Simba waliharibu viti 152 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Kiyovu Machi 4, mwaka huu kabla ya mashabiki wanaodhaniwa wa Yanga kufanya uharibifu kama huo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Azam, Jumamosi iliyopita.

Mkurugenzi wa wizara hiyo, Leonard Thadeo amesema wizara imesikitishwa na muendelezo wa vurugu hizo na inalaani vikali vitendo hicho, hivyo TFF itawajibika kulipa shilingi milioni 10 iwapo uharibifu utatokea hata kama kitaharibika kiti kimoja.

“Katika jitihada za kuendeleza kudhibiti hali hiyo, Wizara imeiagiza TFF kulipa jumla ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya gharama za matengenezo ya viti 130 vilivyovunjwa kwenye mechi ya Yanga dhidi ya Azam wiki iliyopita,” alisema Thadeo.


Khadija Mngwai, GPL

No comments:

Post a Comment