Tuesday, January 31, 2012

MGOMO MADAKTARI, 201 WAAGA DUNIA


MGOMO wa madaktari unaoendelea nchini tangu Jumatatu ya wiki iliyopita, inasemekana umesababisha vifo vya wagonjwa wanaokadiriwa kufikia 201.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya Uwazi tangu mgomo huo ulipoanza, umegundua kwamba kiasi hicho cha wagonjwa waliokufa ni katika mikoa inayokabiliwa na tatizo hilo la madaktari kugoma.
Waandishi wetu Dar es Salaam, walitembelea wodi kadhaa na vyumba vya kuhifadhia maiti vya Hospitali za Temeke, Amana, Mwananyamala na Muhimbili kujionea athari za mgomo huo, huku wa mikoani nao walifanya hivyo.

MUHIMBILI
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, umebaini kuwa wagonjwa wengi wameathiriwa na mgomo huo hali iliyowafanya wajazane wodini bila kupata tiba.

Aidha, timu yetu ilishuhudia wagonjwa wengi wakiwa wamelala chini kwenye korido huku wakiugulia maumivu kwa kukosa huduma ya madaktari.

Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Samson Maandizi, aliyelazwa Wodi ya Sewahaji alisema tangu alipofika hospitalini hapo kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali ya gari, hajawahi kupata matibabu.

Kufuatia hali tete ya kimatibabu iliyosababishwa na mgomo huo, baadhi ya wananchi wamelazimika kuwahamisha wagonjwa wao na kuwapeleka katika hospitali binafsi.

Hata hivyo, mwananchi mwingine, Hamisi Juma alipohojiwa na gazeti hili hospitalini hapo alisema: “Kutokana na kutokuwa na fedha nimeamua kumhamisha mama yangu na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji Mbagala.”

Kwa upande wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo, mhudumu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kwamba tangu mgomo huo uanze idadi ya waliokufa mpaka juzi (Jumapili) wanaweza kufikia 57.

MWANANYAMALA
Kwa upande wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala, mmoja wa wahudumu alisema kwamba idadi ya waliokufa kwa kipindi hicho wanaweza kufikia 20.

AMANA
Katika Hospitali ya Amana mhudumu wa chumba cha maiti amesema tangu mgomo huo ulipoanza, watu waliofariki wanaweza kufikia 15.

TEMEKE
Nayo Hospitali ya Temeke hali ni tete kwani inadaiwa nako wagonjwa 19 wamefariki dunia kipindi cha mgomo, kwa mujibu wa mtumishi mmoja wa hospitali hiyo.

BUGANDO MWANZA
Katika Hospitali ya Bugando Mwanza, mmoja wa wahudumu wa chumba cha maiti alimwambia mwandishi wetu mjini humo kwamba kipindi hiki cha mgomo, wagonjwa waliofariki wanaweza kufikia 25.

MBEYA
Mwandishi wetu wa Mbeya, Gordon Kalulunga, anaripoti kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo wagonjwa wanaofikia 22 walipoteza maisha na wengine walitoroshwa na ndugu zao wakiwa na dripu baada ya kuona hali zao ni mbaya.

DODOMA
Mwandishi wetu Dodoma anaripoti kuwa mgomo huo umesababidha adha kubwa kwa wagonjwa na inakadiriwa watu tisa wamefariki dunia huku wengi wakirudishwa majumbani kwao.

MOROGORO
Mwandishi wetu, Dunstan Shekidele anaripoti:
Kwa mujibu wa mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro aliyeomba jina lake lihifadhiwe, watu wanaokadiriwa 14 wamefariki dunia tangu mgomo huo ulipoanza.
“Kuna baadhi ya ndugu wamewaondoa wangonjwa wao wakiwa na dripu, kwa kweli hali ni mbaya, tumeambiwa wengine wanafia majumbani,” alisema mhudumu huyo.

KIGOMA, IRINGA NA TANGA
Waandishi wetu katika mikoa hiyo wameripoti vifo idadi yake katika mabano kama ifuatavyo;
Kigoma (nane), Bombo mkoani Tanga (nane) na Iringa (saba).

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda ilikuwa akutane na madaktari Jumapili iliyopita kuzungumzia mgogoro huo lakini ikashindikana kwani Mwenyekiti wa Madaktari, Ulimboka Stephen aliliambia gazeti hili kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilichelewesha barua ya mwaliko.

Madaktari hao wameitisha mgomo wakidai kuongezewa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu hatarishi , nyumba na usafiri wa kwenda na kurudi kazini.


Na Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa

No comments:

Post a Comment