Monday, December 12, 2011


MWANAMUZIKI kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ipupa Nsimba ‘Fally Ipupa’ (pichani) amezua bonge la timbwili jijini hapa baada ya shoo yake kuvurugika kufuatia vurugu za mashabiki waliotaka kumpa kipigo.

CHANZO NI MATATIZO YA UMEME
Fally Ipupa anayependwa zaidi na wanawake alitarajiwa kuangusha shoo katika Ukumbi wa Matongee ulipo katikati ya Jiji la Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita (Ijumaa), lakini alishindwa kutokana na matatizo ya umeme.

JENERETA LASHINDWA KUFUA DAFU
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na ‘kachero’ wetu, hata baada ya waandaaji kufanya mpango wa jenereta kubwa, bado mambo hayakwenda sawa kwani lilishindwa kuwasha vyombo vya muziki vya Fally Ipupa.

Kufuatia hali hiyo, liliibuka bonge la varangati kutoka kwa mashabiki waliotoa buku 15 na wengine 30 wakitaka warudishiwe chao kabla ya kutoa uhai wa mwanamuziki huyo.

Timbwili hilo lilisababisha hasara kubwa kwani baadhi ya mashabiki walishuhudiwa wakiondoka ukumbini hapo na viti vitatu kwa kila mmoja huku Fally Ipupa akiishia mikononi mwa polisi kwa ajili ya usalama wa kumuondoa mahali hapo.

LAWAMA
Kwa mujibu wa mratibu wa shoo hiyo aliyetajwa kwa jina la Dativus Mango, shoo hiyo ilivurugika na kushindwa kufanyika kutokana na sababu ya umeme kuwa mdogo huku akitupia lawama uongozi wa Ukumbi wa Matongee.

Alisema kuwa hasara iliyotokana na vurugu hizo ni kubwa ikiwa ni pamoja na kulipia ukumbi Sh. milioni 1.2, malipo ya Fally Ipupa Euro 25,000 (zaidi ya Sh. milioni 50) na gharama nyingine kibao.

FALLY IPUPA ADHALILISHWA
Kwa upande wake Fally Ipupa alisema alisikitishwa ile mbaya na tukio hilo akiweka wazi kuwa alidhalilika kwa mashabiki wake.

UONGOZI WA MATONGEE
Akizungumzia varangati hilo, Mkurugenzi wa Matongee, Sombyo Lebi alisema ukumbi huo ulipata hasara kubwa ikiwemo upotevu wa viti 1700 na rasilimali nyingine za ukumbi huo huku akiwashukuru polisi mkoani hapa kwani kama siyo wao, leo tungezungumza mengine.


Na Joseph Ngilisho, Arusha, GPL

No comments:

Post a Comment