MVUTANO mkubwa umeibuka baina ya jamii ya wafugaji (wanaoabudu mila na desturi) na wachungaji wa madhehebu mbalimbali ya kidini wilayani Arumeru na kusababisha baadhi ya wachungaji kuzikimbia familia zao wakihofia kuuawa. Katika hali isiyokuwa ya kawaida mchungaji wa kanisa la Matendo, (Pentekoste),Julius Lukumay (34)amekiona cha moto baada ya kujikuta akitembezwa uchi wa mnyama kwa siku mbili mfululizo na jamii hiyo ya wafugaji kwa madai ya kukataa kushiriki kikao cha kimila. Ilidaiwa ya kuwa adhabu hiyo imetokana na mchungaji Lukumay kukaidi kulipa faini ya shilingi 500,000 aliotozwa na jamii hiyo kwa kile kilichoelezwa kwamba aliwashitaki wazee wa kimila katika ofisi ya mtendaji wa kijiji cha Siwandeti wilayani humo akiwatuhumu kuendesha mambo mbalimbali yasiyofaa. Hali hiyo imesababisha wachungaji wengine zaidi ya 7 wa makanisa ya kipentekoste kutimka majumbani kwao na kukimbilia kusikojulikana ,wakihofia kukamatwa na kupewa adhabu kama hiyo ya kutembezwa uchi na jamii hiyo ya wafugaji, ambapo kwa muda mrefu jamiia hiyo na wachungaji wamekuwa hawaivani. Mchungaji Lukumay anadai kutembezwa uchi akiwa amefungwa kengere na bati lenye maandishi shingoni, katika vijiji vya Mringaringa,Kiranyi ,Kemnyaki,Ngaramtoni ,Olevolosi , Eleray huku vijana hao wanaodaiwa kuamuriwa na wazee wa mila wakimwimbia nyimbo za kumkejeri. Udhalilishaji huo kwa viongozi wa dini umekuwa ukijirudia mara kwa mara wilayani humo , ambapo miaka kadhaa iliyopita ,wakazi wa maeneo hayo wanakumbukumbu ya mchungaji mwingine kufanyiwa vitendo vya kinyama kwa kutembezwa uchi huku kundi la vijana na watoto wakimdhihaki kwa nyimbo na maneno ya kejeri,akituhumiwa kupinga tohara. Akizungumza na wandishi wa habari alipokuwa amelazwa katika hospitali ya Seliani ,iliyopo eneo la Ngaramtoni baada ya kupata majeraha kadhaa ya kupigwa na kuishiwa nguvu,Lukumay alisema kuwa watu hao wamemdhalilisha sana baada ya kumvua nguo zote kisha kimtembeza uchi mbele ya watoto wadogo. ''kwa kweli wamenidhalilisha sana ,kwanza mimi ni mlokole nina familia na watoto wanne nampenda yesu ,nilishawaambia dini zetu haziruhusu kuingiliwa na mambo ya kimila,sasa hawaelewi wanashindwa kutengenisha masuala ya kidini na mila za asili ''alisema Lukumay huku akionyesha majeraha kadhaa yaliyotokana na kipigo. Mchungaji huyo alidai kwamba,polisi waliofika eneo hilo siku ya pili ndiyo waliomwokoa, kwani bila wao bila shaka mauti yangemfika kwa kuwa watu hao walikuwa na dhamira mbaya maana walimpiga na kumburuza kama alivyofanyiwa yesu Masiha na Wayahudi. Aidha ameiomba serikali kuingilia kati kwa kuwa mila za makabila hayo zimekuwa zikitumika vibaya ikiwemo kuwanyanyasa pale inapobainika kwamba wamejitenga na mila hizo na kuokoka. Nae katibu wa umoja wa wachungaji wa madhehebu ya kipentekoste,Joseph Kaondo amelaani kitendo hicho na kulitupia lawama jeshi la polisi kwa madai kwamba limeshindwa kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa watumishi wa mungu . Alisema wazee jamii ya wafugaji ndio wamekuwa wakiongoza kuwaamuru vijana kufanya msako dhidi ya wachungaji na kuwakamata , kisha kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji bila kuchukuliwa hatua zozote. Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Akili Mpwapwa alikiri kupata taarifa hizo na kudai kwamba anazifanyia kazi ikiwepo kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ''ni kweli nimepata taarifa ila sisi kama polisi tunafanya uchunguzi ili kujua undani wa tukio hilo''alisema.
NA GLADNESS MUSHI WA FULLSHANGWE -ARUSHA
NA GLADNESS MUSHI WA FULLSHANGWE -ARUSHA
No comments:
Post a Comment