Friday, November 18, 2011


KAMA ingekuwa sinema, basi muvi ya kuvunjika kwa ndoa ya Irene Pancras Uwoya (pichani) na Hamad Ndikumana ‘Kataut’ ingeshinda tuzo ya mwaka 2011 kufuatia mshtuko wake, Ijumaa limechimba siku 822 za mapenzi yao na kubaini siri nzito nyuma ya pazia, shuka nayo.

Ukiacha sababu iliyotolewa na Uwoya mbele ya gazeti damu moja na hili, Risasi Mchanganyiko toleo namba 852 la Jumatano Novemba 16-18, mwaka huu kuwa hakumpenda Kataut na ana mtu mwingine anayempenda, kuna sababu nyingine tano zilisababisha ndoa hiyo kuvunjika.

Katika safari ya ndoa waliyoianza Julai 11, 2009 kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam ambayo ilimalizika usiku wa kuamkia Jumatatu ya Novemba 14, 2011 ikiwa ni siku 822, ilibainika kuwa Uwoya hakuwahi kufurahia maisha ya ndoa kwa sababu zifutazo;

MOSI: UWOYA ALITAKA UHURU, AKAUKOSA
Mara kadhaa Uwoya aliwahi kukiri kuwa ndoa hiyo ilikuwa ikimnyima uhuru wa kufanya mambo yake binafsi na kujiachia atakavyo ikiwa ni pamoja kutokauka katika kumbi za starehe.

Wiki moja baada ya kujifungua mtoto wa kiume, Krish, Mei 8, 2010 (yuko kwa bibi yake, mama wa Uwoya) Uwoya alinukuliwa: “Natamani kwenda klabu, lakini nashindwa kwa sababu ya mtoto na ndoa yangu.”

PILI: NGUMI KILA KUKICHA
Kwa mujibu wa majirani wa Uwoya maeneo ya Mbezi Jogoo, Dar, wawili hao walikuwa wakitofautiana kila kukicha huku wakizitwanga ngumi hadi kugeuka sinema mtaani hivyo kuchochea moto wa kutengana.

Katika gazeti pacha la hili, Ijumaa Wikienda toleo namba 237 la Jumatatu Novemba 14-20, mwaka huu, Uwoya aliripotiwa kuchezea kichapo kibaya kutoka kwa Kataut ndipo akaapa kwamba hatapigwa tena.

TATU: WIVU WA KUPITILIZA WA KATAUT
Ilibainika kuwa Kataut alikuwa na wivu kupitiliza kwa Uwoya ndiyo maana alikuwa hachezi mbali na simu ya Uwoya na alipokutana na ‘SMS mbovumbovu’ kutoka mwanaume, hali ya hewa ilichafuka.
Kuhusu hilo, Uwoya aliliambia Ijumaa: “Asikwambie mtu, tatizo Hamad (Kataut) alikuwa na wivu wa kufa mtu.”

NNE: MADAI YA NDIKUMANA KUWA NA MWANAMKE MWINGINE
Katika nusanusa ya gazeti hili ilibainika kuwa Kataut alikuwa na mwanamke mwingine kabla ya Uwoya aliyezaa naye.
Kuhusu hilo, Uwoya alisema: “Ni kweli alikuwa na mwanamke mwingine anayeishi Uingereza, lakini aliniambia walishaachana hivyo sikuona tatizo sana.”

TANO: KATAUT KUHAMIA BONGO
Ilibainika kuwa Uwoya alikuwa hapendi kuishi Cyprus kwa mumewe kutokana na hali ya hewa, hivyo alikuwa akirudi Bongo mara kwa mara kwa kisingizio cha kuigiza, jambo ambalo lilimfanya Kataut kufuatana naye, lakini yeye hakupenda na aliona ni kero.
Ilisemekana kuwa kitendo cha Kataut kuhamia ukweni kilizidi kuchochea wawili hao kutengana kwani siyo utamaduni wa Kitanzania mwanaume kukaa ukweni.

MASTAA HAWAAMINI
Baada ya habari ya Uwoya kuwa gumzo mtaani, Ijumaa lilizungumza na mastaa mbalimbali wa Bongo ambao walieleza kushtushwa na habari hiyo.

KULWA KIKUMBA ‘DUDE’:
“Ni jambo la kusikitisha, wasanii tumeaibika sana, tunaonekana sisi siyo watu wa kudumu katika ndoa zetu, inauma kupita maelezo. Namuomba Mungu warudiane.”

JACOB STEVEN ‘JB’:
“Nimechukia sana kwani alichokiunganisha Mungu, mwanadamu hawezi kukitenganisha. Nitapiga magoti nimuombe Mungu ili ndoa yao irudi kama zamani.”

JACQUELINE WOLPER:
“Nasikitika na naogopa sana kwa sababu wasanii tutakimbiwa na kuonekana hatufai. Nawaomba chondechonde warudiane jamani.”

AUNT EZEKIEL:
“Jamani inauma sana, kikubwa tuwaombee ili shetani apite mbali waendelee kukaa kama walivyokuwa mwanzoni.”

BELINA MGENI:
“Nimeumia sana, nawaombea kwa Mungu waweke mambo sawa, ndoa yao irudi kama zamani.”

BLANDINA CHAGULA ‘JOHARI’:
“Ukweli inauma sana, naomba waweke mambo sawa kwani tunatamani kuwaona tena pamoja.”

SHAMSA FORD:
“Mimi niko hoi kwa taarifa hiyo kwani nimeumia sana. Nawaomba warudiane jamani.”

STEVEN KANUMBA:
“Tafadhali naomba mnipe muda nitalizungumzia suala hilo.”

RAY NA CHIKOKA
Hawa ni mastaa ambao ni watu wa karibu wa Uwoya ambao mara nyingi hufanya naye kazi. Juhudi za kuwapata ili kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda.

KATAUT VIPI?
Juhudi za kumpata Kataut ili kuzungumzia kuvunjika kwa ndoa yake bado zinaendelea hivyo usikose nakala yako ya Ijumaa Wikienda Jumatatu ijayo.

NENO LA IJUMAA
Timu ya Ijumaa inasikitishwa na habari ya kuvunjika kwa ndoa hiyo na imekuwa ikifanya juhudi za kuweka mambo sawa kwani hakuna linaloshindikana chini ya jua na inatamani kuwaona wawili hao wakiwa pamoja.


Na Imelda Mtema, GlobalPublishersTz

No comments:

Post a Comment