Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel, Prof Wangari Maathai, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.
Mwanaharakati huyo mashuhuri wa mazingira na haki za binadamu wa Kenya, amefariki mjini Nairobi usiku wa kuamkia Jumatatu kutokana na maradhi ya saratani.
Prof Karanja Njoroge ambaye ni Mkurugenzi wa Green Belt Movement, shirika ambalo Prof Maathai alilianzisha, amethibitisha kifo hicho.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Prof Njoroge amesema wakati wa kifo chake Wangari alikuwa na wanafamilia na marafiki.
Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike.
Profesa Wangari Maathai alipata Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Mbali ya kuwa mwanaharakati wa masuala ya mazingira na haki za binadamu , Maathai alikuwa pia mwanasiasa shupavu. Amewahi k mbunge na naibu waziri wa mazingira nchini Kenya.
Wakati wa uhai wake, alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.
Mwanamke huyo shupavu, alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.
Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili ambapo shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani.
Maathari alizaliwa Aprili 1, 1940 huko Nyeri, Kenya, na alikuwa mwanamke wa kwanza wa Afrika kupata Tuzo ya Anabu ta Nobel.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Mt. Scholastica mwaka 1964 na baadaye Chuo Kikuu cha Pittsburgh mwaka 1966,aliporejeaKenya na kupata shahada ya uzamili (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi 1971.
Baada ya hapo alifanya kazi kama Profesa katika Idara ya Madawa ya Wanyama kabla ya kuanzisha Harakati za Green Belt za kupanda miti ili kuzuia uteketezaji wa misitu na kutoa nishati ya kuni na wanawake wa Kenya.
Aligombea urais wa Kenya pamoja na ubunge mwaka 1997 lakini hakufanikiwa.
Mwaka 2002 Desemba akafanikiwa kuchaguliwa na kuwa mbunge, na mwaka 2003 akateuliwa na Rais Mwai Kibaki kuwa Waziri wa Mazingira, Maliasili na Wanyama Pori.
Na Global Publishers Tz
No comments:
Post a Comment