Saturday, September 17, 2011

Jaji aliyemhukumu Nguza "Babu Seya" akana tuhuma kuwa alishinikizwa na Kiongozi mmoja wa Serikali.



Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Thomas Mihayo, jana aliukana uvumi ulioenea kuwa, kiongozi mmoja mkubwa wa serikali aliwashinikiza majaji ili watoe hukumu ya kifungo cha maisha kwa mwanamuziki mashuhuri nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na watoto wake.

Jaji Mihayo alisema alitenga muda wa kuongea na watoto wasichana waliodaiwa kubakwa na Babu Seya na wanawe na akagundua kwamba watoto hao walikuwa wamelawitiwa na kwamba tendo hilo lilikuwa limefanywa kwa kipindi cha miezi kadhaa.

Alisema aliwasikiliza watoto hao na akapata picha kamili ya kilichoendelea katika matukio hayo na pia aligundua kwamba wazazi wa watoto hao hawakuwa wanajua mwenendo wa watoto wao.

Alifafanua kwamba baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikitoa ripoti isiyo sahihi ya kesi hiyo na akasema kwamba kama waandishi wangefanya uandishi wa kiuchunguzi, wangeweza kupata ukweli wa tukio hilo, “Kibaya ni kwamba waandishi hawakulichunguza tukio hilo kiundani, vinginevyo wangeweza kupata ukweli wenyewe,” alisema Jaji Mihayo.

Alisema uandishi wa kiuchunguzi unakosekana Tanzania na akawaomba wanachama wa vyombo vya habari nchini kusoma hiyo ripoti mpya ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari vya magazeti iliyozinduliwa na MCT kwa nia ya kubaini mapungufu yao katika eneo la kuripoti habari za uchunguzi na kuyasahihisha.

Hivi sasa Babu Seya na mwanaye mmoja, wanatumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kuwalawiti watoto wanafunzi wa kike. Washtakiwa wawili waliachiwa huru na Mahakama ya Rufani.

“Hakika si kweli… Niliupitia mwenendo wa kesi hiyo na kubaini kwamba kilichokuwa kinasemwa mitaani kilikuwa ni uvumi usiokuwa na chembe ya ukweli...,” “Na cha kushangaza, vyombo vya habari vilikuwa vikiutangaza uvumi huu,” alisema Jaji Mihayo alipokuwa akizindua rasmi Ripoti ya Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari vya magazeti (Julai 2010-Juni 2011) ya Baraza la Habari la Tanzania (MCT) jana jijini Dar es Salaam.

Jaji Mihayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya MCT, alisema aliusoma kwa kina mwenendo wa kesi ya kulawiti dhidi ya Babu Seya na wanawe kama ulivyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kabla ya kutoa hukumu ya mwisho.

Alisema kwa kuwa Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kuamua kuhusiana na shauri hilo, ilipokea ukweli wa mwanzo wa shauri hilo na ikauwasilisha Mahakama Kuu, “Kwa kweli ni mimi ndiye nilikuwa mwenyekiti wa kesi hiyo kama Jaji wa Mahakama Kuu na ndiye niliyetoa hukumu ya mwisho (ya kumhukumu Babu Seya na wanaye kifungo cha maisha),” alisema.

Alisema wakati akizisoma nyaraka na mwenendo wa kesi toka katika mahakama hiyo ya chini (Mahakama ya Kisutu), aligundua kwamba kilichokuwa kikisemwa na watu mitaani ulikuwa ni uvumi tu, “Si kweli kwamba kulikuwa na ofisa mmoja mkubwa katika duru za serikali ambaye alitoa shinikizo kwa Majaji lililowafanya wafikie kwenye tamati hiyo ya kumhukumu Babu Seya na wanaye kifungo cha maisha,” alisema.

No comments:

Post a Comment