Wednesday, September 21, 2011

DAR YAICHAPA IRINGA 10-0 MICHUANO YA AIRTEL RISING STARS

Rajab Moto (kushoto) wa Dar akitafuta mbinu za kumtoka Mussa Likwale wa Iringa.

Mussa Likwale (mbele) wa Iringa akiondoka na mpira huku akikabwa na
Hassan Rashid (kushoto) wa Dar.

Mussa Likwale (kushoto) wa Iringa, akiwania mpira na Abdalah Hamis wa Dar es Salaam katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Kulia ni Rajab Mwarami wa Dar ambapo Iringa ilibugizwa mabao 10-0.

MICHUANO ya fainali za kitaifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) maarufu kama Airtel Rising Stars, iliendelea kutimua vumbi Jumapili iliyopita, ambapo timu ya Dar es Salaam ilitoa onyo kali kwa timu shiriki baada ya kuichapa timu ya Iringa mabao 10-0 kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa michuano hiyo ambayo ilianza Jumamosi kwa timu ya Morogoro kuichapa Mwanza 6-0 ambapo timu husika ni kombaini za shule za sekondari za mikoa husika.

Katika mchezo wa Jumapili, dalili za timu ya Dar es Salaam kuibuka na ushindi mnono zilianza mapema ambapo dakika tano za mwanzo wa mchezo huo, washumbuliaji wa Dar es Salaam walikuwa wameshafika langoni mwa wapinzani wao mara tatu huku kipa wa Iringa akifanya kazi kubwa kuzuia mashuti makali yaliyokuwa yakielekezwa langoni mwake.

Hata hivyo, katika dakika ya 10, Dar es Salaam walianza sherehe ya mabao baada Rajabu Mwarami kuandika bao la kwanza. Mnamo dakika ya 22 Omary Abdallah aliipatia Dar es Salaam bao la pili, na kabla wachezaji wa Iringa hawajakaa vizuri, Shaban Mtambo akaongeza bao la tatu dakika ya 24.

Joseph Seleman alifunga goli la nne dakika ya 38 na mpaka timu zinakwenda mapumziko, timu ya Dar es Salaam ilikuwa inaongoza kwa mabao manne.

Mnamo dakika ya 58 ya kipindi cha pili, Joseph Seleman ailiendeleza karamu ya magoli baada ya kufunga goli la tano na dakika ya 69 Omary Abdallah aliongeza goli la sita.

Timu ya Iringa, ambayo kwa haikuonyesha jitihada za kutia moyo, iliendelea kuruhusu nyavu zao kutikiswa dakika ya 72 mfungaji akiwa ni Rajabu Moto na dakika tatu baadaye Alphonce Mkunde alifunga goli la nane. Goli la tisa na kumi yalifungwa na Amos Nguti na Abdalatif Hamis.

Michuano hiyo ambayo imedhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na llabu ya Manchester United ya Uingereza inaendelea tena leo Jumanne ambapo Morogoro watacheza na Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment