Friday, September 16, 2011


BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga baada ya kuanza na mwendo wa pole jana imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza kwa kuichakaza African Lyon mabao 2-1 katika mchezo wa ushindani uliofanyika kwenye Uwanja wa Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.

Yanga ambayo kutokana na ushindi huo imefikisha pointi sita ilifanikiwa kupata mabao yake kupitia kwa Mzambia Davies Mwape na Mtanzania Rashid Gumbo.

Akielezea tathmini yake mara baada ya mchezo huo Kocha wa Lyon, Jumanne Charles alisema “Vijana wangu wamecheza vizuri, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata, hata hivyo Juma Seif (kipa wake) hakuwa makini langoni.”

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Sam Timbe alisema: “Sina cha kuongea”.
Katika mchezo huo ulioanza kwa kasi, Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi la nguvu kwa wapinzani wao katika dakika ya 14, ambapo Mwape alikosa bao la wazi baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Lyon kutokana na kona iliyopigwa na beki Shadrack Nsajigwa.

Mwape alianza kuandika bao hilo katika dakika ya 35 akiunganisha krosi iliyopigwa na Shamte Ally. Halikudumu sana, kwani dakika mbili kabla ya mapumziko Khamis Shengo aliisawazishia Lyon kwa shuti la faulo lililogonga mwamba kisha kujaa wavuni.

Katika dakika ya 63, Gumbo alipata pasi nzuri kutoka kwa Abuu Ubwa, kisha akawapangua walinzi wawili wa Lyon na kupiga shuti umbali wa mita 20 ambalo moja kwa moja likaingia ndani ya lango.

Katika mechi hiyo Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Shamte, Kigi Makasi, Juma Seif ‘Kijiko’ na kuingia Kenneth Asamoah, Gumbo na Godfrey Bonny.

Na Wilbert Moland na Khatimu Naheka, Global Publishers Tz

No comments:

Post a Comment