Thomas Mashalla, Arusha
WAKILI maarufu jijini Arusha, anadaiwa kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na kiasi kikubwa cha fedha kwenye akiba yake binafsi, zinazodaiwa kuingia kwa njia isiyo halali.
Wakili huyo aliyejijengea umaarufu nchini kutokana na uendeshaji kesi zake, anadaiwa kukamatwa Agosti 2, mwaka huu wakati akiendesha gari lake la kifahari aina ya Escalade, Polisi wa Kimataifa Interpol walishikilia kabla ya kumfikisha Kituo Kikuu cha Polisi.
Taarifa zilipatikana zinadai ya kuwa, kushikiliwa kwa wakili huyo kunafuatia polisi nchini kufuatilia nyendo zake kwa kipindi kirefu kuhusiana na shughuli zake, huku wakihofia kiasi kikubwa cha fedha kilichokutwa kwenye akaunti yake binafsi kwenye benki moja nchini.Pia, taarifa hizo zinadai wakili huyo alikamatwa majira ya usiku na kwamba, kabla ya Interpol kumfikisha Kituo Kikuu cha Polisi walifanya upekuzi kwenye nyumba yake iliyopo mkoani Arusha.
Vyanzo vya habari vinadai kuwa, baada ya polisi hao kufanya upekuzi wa kina sehemu hizo mbili walimfikisha Kituo Kikuu cha Polisi ili kuruhusu hatua nyingine kufuata.Taarifa zinadai kuwa, wakati anakamatwa ndani ya gari alikutwa na zaidi ya Sh20 milioni na kwamba, baada ya kumhoji juu ya kiasi hicho cha fedha, inadaiwa aliwajibu hizo zilikuwa kwa ajili ya matumizi yake madogo.
“Walimkamata akiwa anaendesha gari lake hapa mjini, lakini ndani ya gari walikuta Sh20 milioni, walipomuuliza aliwajibu kuwa hizo ni kwa ajili ya matumizi yake madogo madogo,” kilisema chanzo cha habari. Inadaiwa chanzo cha polisi kufuatilia nyendo zake, inatokana na akiba ya wakili huyo kukutwa na kiasi cha zaidi ya Sh30 bilioni zinazodaiwa kuingizwa njia zisizo halali.
Pia, inadaiwa polisi walikuwa na mashaka na gari analotumia kuingizwa nchini kinyemela.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, hakukiri wala kukataa zaidi ya alisema suala hilo liko ngazi za juu, hawezi kuzungumzia.
“Kwa kweli hilo suala liko juu ya ngazi yangu, siwezi kulizungumzia chochote kwa sasa hadi nipate idhini kutoka kwa wakubwa wangu,” alisema Andengenye.
Andengenye alisema anasubiri taarifa kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na akipata kibali atalitolea ufafanuzi.Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) tawi la Arusha, Duncan Ooola, alikiri kukamatwa kwa wakili huyo na kwamba, walipofuatilia waliambiwa anachunguzwa na polisi.
“Ni kweli wamemkamata (jina tunalo) Jumanne, lakini sijui saa ngapi, tulikwenda polisi kujua chanzo walitwambia anachunguzwa, hiyo ndiyo taarifa ninayoweza kukupa,” alisema Ooola.
No comments:
Post a Comment