Friday, August 12, 2011

Na Saleh Ally
KAMA ambavyo imekuwa gumzo Ulaya, mishahara ya wachezaji wa Simba inaweza kuzua gumzo kubwa hapa nchini.

Ingawa inapishana sana kwa kuwa ndiyo utaratibu ulivyo kwenye sehemu za ajira hapa Tanzania na kwingineko dunia, mshambuliaji wake Felix Sunzu kutoka Zambia ndiye kinara kwa upande wa wageni wakati kiungo mpya, Mwinyi Kazimoto anashika usukani kwa wenyeji.

Sunzu ameweka rekodi kutokana na mshahara wake wa dola 3,500 (zaidi ya Sh milioni 5.2), ndiye analipwa zaidi Ligi Kuu ya Vodacom. Rekodi hiyo, msimu uliopita mshambuliaji wa Azam FC, Kali Ongala aliyekuwa akilipwa dola 4,000, sasa ni kocha msaidizi wa timu hiyo.

Kwa upande wa wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Gervais Kago anafuatia kwa kuchukua dola 1,000 (Sh milioni 1.5), akifuatiwa na Emmanuel Okwi (dola 800 au Sh milioni 1.2) baada ya mkataba mpya. Jerry Santo na Mafisango wanalipwa kila mmoja dola 500 au Sh 750,000.

Hao ndiyo wachezaji watano wa kigeni, kwa upande wa wale wa nyumbani, Kazimoto ambaye ametokea JKT Ruvu analipwa Sh milioni moja, akifuatiwa na ‘mafadha’ wawili, Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’, kila mmoja Sh 800,000.

Mshambuliaji Mussa Mgosi amejiunga na DCMP ya DR Congo hivi karibuni, lakini wakati yupo Msimbazi alikuwa akichukua Sh 750,000. Mbwana Samatta aliyeenda TP Mazembe alikuwa akilipwa Sh 600,000.

Asilimia kubwa ya wachezaji waliopo Msimbazi kama Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Mohammed Banka ambaye amevunja mkataba wamekuwa wakilamba Sh 500,000 huku baadhi kama Amir Maftah, Shija Mkina, Juma Jabu, Uhuru Selemani, All Mustapha BArthez wakilamba kuanzia Sh 300,000 hadi 450,000.

Wachezaji makinda, wakiwemo wale waliopandishwa kutokea timu B wamekuwa wakilipwa Sh 150,000 hadi 200,000.

Ukiachana na mfumo wa zamani, kampuni nyingi zimekuwa zikilipa mshahara tofauti kulingana na uwezo wa kikazi wa wafanyakazi wake, pia kwa kutegemea yalivyokuwa majadiliano ya kwanza wakati wakiingia mikataba.


Source: Global Publishers Tz

No comments:

Post a Comment