Na Khadija Mngwai, Global Publishers
MSHAMBULIAJI Mussa Mgosi amesema kuwa, alipata mapokezi ya kifalme alipotua kwenye timu yake mpya ya DC Motema Pembe ya DR Congo.
Mshambuliaji huyo aliuzwa na Simba ya jijini Dar es Salaam kwenda kwenye kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Congo hivi karibuni.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mgosi alisema kuwa, kupata nafasi katika klabu ya Motema Pembe siyo mwisho wake, hivyo anahitaji kuongeza juhudi zaidi ili aweze kusonga mbele kisoka.
“Kwa kweli mapokezi niliyopata yamenifurahisha sana, viongozi pamoja na mashabiki wameonyesha kuwa wananihitaji klabuni kwao, walinipokea vizuri kama mfalme.
“Nafasi hii ni adimu sana, kwani siku zote malengo yangu yalikuwa kucheza nje ya nchi na sasa naona safari imeanza.
“Cha msingi ni kuongeza juhudi katika kufanya mazoezi ili kiwango kiendelee kuwa juu.
“Naamini kuwa, nikiongeza juhudi nitakuwa bora zaidi ya hapa na nitapata nafasi ya kucheza kwenye timu kubwa zaidi ya hii,” alisema Mgosi baba wa watoto wawili.
Mgosi amesajiliwa na Motema Pembe hivi karibuni kwa kitita cha dola 15,000 (zaidi ya shilingi milioni 20), sasa yupo hapa nchini akijiandaa kukamilisha baadhi ya mambo yake kabla hajarejea Congo kuanza kazi.
No comments:
Post a Comment