Monday, July 11, 2011

ZANZIBAR KUANZISHA SHIRIKA LAKE LA NDEGE

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema iko mbioni kuanzisha shirika lake la ndege, badala ya kuendelea kutegemea mashirika ya nje, jambo ambalo halisaidii zaidi kutoa ajira kwa wananchi wake.

Akizungumza na gazeti MTANZANIA Jumapili mjini Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema taratibu na hatua zote za kuanzishwa kwa shirika hilo, zinaendelea vizuri, “Hivi sasa tuna mipango madhubuti ya kuanzisha shirika letu la ndege ambalo tunaamini litakuwa mkombozi mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga na hata kutoa ajira kwa Wazanzibari waliosomea fani hiyo,” alisema Maalim Seif.

Alisema sababu ya pili ya iliyofanya SMZ ifikie uamuzi huo, ni kutokana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kukosa mwelekeo kwa kipindi kirefu na kuacha mashirika ya nje kuendelea kutamba katika safari za anga, “Tulikuwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), lakini katika miaka ya karibuni limekuwa katika wakati mgumu wa kujiendesha na kuacha mashirika ya nje yakiendelea kufanya vizuri,” Maalim Seif alisema na kuongeza, “Tunagemea uuanzishwaji wa shirika letu utasaidia kupunguza tatizo hili, tunataka kuona tunapiga hatua kubwa katika hili, tulitegemea ATC ingekuwa kiungo kizuri katika sekta hii, lakini naona mambo si mazuri... “Hapa Zanzibar tunapokea wageni wengi, tunaamini kuwa na shirika letu kutasaidia zaidi kututangaza na kuleta wageni wengi ambao wamekuwa wakitembelea visiwa vyetu kila mwaka,njia hii kwanza itatusaidia kuungana na mashirika mengine ya kimataifa.”

Alisema kutokana na wananchi wengi wa Zanzibar kutegemea biashara, ni wazi watafungua milango zaidi na wafanyabiashara wa nje ambao wanapenda kuendesha biashara zao katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema hivi sasa wameanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya watu wa China, ambapo utawezesha ndege kubwa kutua na kuruka bila wasiwasi wowote ule.

source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/07/zanzibar-kuanzisha-shirika-lake-la-ndege.html#ixzz1RmdQh6ka

No comments:

Post a Comment