Tuesday, July 19, 2011

TIBA KWA BABU AMBI KWISHNEI

Na Haruni Sanchawa
Mch. Ambilikile Masapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo amebadili upepo na sasa yupo ‘bize’ kujenga nyumba yake.

Chanzo chetu cha habari kijijini hapo, kilisema Babu amekuwa akijenga nyumba yake baada ya wateja kupungua.

“Wateja wa Babu wamepungua sana wengi wanaokuja wanatoka nje ya nchi. Hivi sasa siyo yule ambaye alikuwa akifanya kazi mpaka usiku. Muda mwingi anakuwa akijenga, ni mtaalamu wa ujenzi,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilipoulizwa kwa wastani Babu anatibu watu wangapi, kilisema si wengi sana. “Siyo vizuri kusema idadi, lakini ukiona mtu anaacha tiba na kwenda kujenga elewa kwamba wateja ni wachache sana,” kilisema.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaomzunguka Babu wanamshukuru kwa sababu kawaletea maendeleo.

“Hivi sasa tuna minara ya mitandao, barabara kutoka Arusha imetengenezwa kwa ajili ya Babu, tunamshukuru sana. Hata akibadili upepo na kuamua kuendelea na fani ya ujenzi, sisi hatumlaumu.

Sasa afanye nini na wateja hawaji kwa maelfu?” alisema mwanakijiji mmoja aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.

Mchungaji Masapile amejipatia umaarufu mkubwa baada ya kudai kuoteshwa dawa na Mungu ambayo alisema inatibu magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi.

No comments:

Post a Comment