Friday, July 1, 2011

Nchi Ya Wapiga Porojo Itaendelea Kwa Muujiza Upi?

Kama kuna jambo linalowaumiza vichwa watanznia basi ni swali kuwa kwanini kila wanalopanga halifanikiwi? au kwanini wananchi ni masikini licha ya maliasili zilizojaa kila kona yanchi hii? Wakiangalia elimu hoi watoto wanafeli, wakija kwenye afya hakuna kitu, wakienda kwenye kilimo na hata umeme tabu tu kwa kifupi hakuna jipya ni uduni na ubabaishaji mtupu.

Katika lindi la mawazo ya namna hii au maswali mengi yasiyojibika tunawatazama viongozi wetu na uwajibikaji wao usiokidhi viwango kiasi kwamba wamepwaya mno , wajuzi wa kuzungumza bila kutenda, ni watu wa blah blah na porojo tu.

Kwakweli Tanzania imetawaliwa na wapiga porojo hebu angalia kwenye hiyo kaulimbiu ya “kilimo kwanza”inavyotangazwa na kupigiwa chapuo na viongozi wetu kasha nenda huko vijijini kwenye mashamba utaona hata mabwana shamba hakuna na hizo pembejeo zenyewe za kilimo hakuna, sasa utasema hapo kuna kilimo kwanza au porojo tu?

Geukia elimu nddio utashangaa kabisa kulivyooza huko lakini cha ajabu ni kuwa viongozi wetu bado wna ujasiri wa kusimama kwenye majukwaa na kudai kuwa serikali imeboresha elimu, elimu gani? Shule za kata? Si ndio hizi zinatoa sifuri? Nasikia siku hizi zinaitwa mtambo wa sifuri, ajabu sana! Yaani serikali inajenga majengo tupu bila walimu,madawati wala maabara kasha wanaita sekondari halafu wanazidi kuboronga wanafuta mitihani, tuziiteje hizi? Hizi ni porojo za watawala wetu, porojo porojo kila mtu anapiga porojo tu.
Njoo kwenye hizo huduma za afya , tunaambiwa kuwa Tanzania bila maralia inawezekana tena kwa mbwembwe kwa matamasha makubwa lakini hivi mtu wa kule kijijini analala chini hana hata hiko kitanda je hiyo neti atachomeka wapi? Au motto wa mtaani analala kwenye vichochoro huyu neti atachomeka wapi? Sasa hizo Zahanati za vijijini kama kweli zinaviwango mbona vifo vya akina mama wajawazito bado vinaendelea? Hakika hizi ni porojo za viongozi wetu!

Halafu anaibuka kiongozi mkubwa wa nchi anadai msongamano wa magari jijini Dar es salaam ni ushahidi wa kukua kwa uchumi wetu, hizi sasa porojo, uchumi wetu na nani? Mafisadi? Au Brigedia Al Adawy na Dowans? Uchumi umekua na ombaomba wameongozeka ndiyo magari yameongezeka na umasikini umekithiri , sasa huo uchumi uliokua umemnufaisha nani? Mawaziri na wabunge? Au rais na waziri mkuu? Hizi ni porojo tupu.

Serikali nayo imeshindwa kuweka huduma za nishati ya umeme wa uhakika, sasa naona ina mchoko naam! Huu ni mchoko ndio maana kila kwenye hotuba tunapigwa kalenda mpaka mwaka huu au ule tatizo la umeme litakuwa historia halafu mda huohuo umeme ni wa mgao, waziri wa nishati nay eye hana jipya bado watu tunateseka kwa sababu ya kukosa ubunifu na uzalendo , mwenyekiti wa kamati ya bunge ya nishati anataka tuwashe mitambo ya Dowans, watu wanahoji anataka turudi tulipotoka? Hizi kama sio porojo nini basi? Nchi ipo gizani viongozi wanapiga porojo inasikitisha sana.

Tabia ya kupiga porojo inaendelea kudidimiza nchi , hata kwenye michezo tunapiga porojo halafu tunataka kucheza kombe la Dunia,bungeni kuna porojo kiasi kwamba bunge linafanywa sehemu ya kupigana vijembe na mipasho halafu na sisi tunaamini iko siku tutakuwa kama wenzetu wa Ulaya na Marekani ambao tayari wamefuta blah blah na porojo kwenye kamusi za vichwa vyao wanafanya mambo kizalendo na kwa kujituma, haiwezekani !

Matokeo ya porojo yanapoonekana viongozi wetu hawachelewi kusikitika na kuhidi kujirekebisha, ona matokeo ya kidato cha nne yalivyowaumbua viongozi sasa wanajifanya wamejifunza hakuna kitu porojo tu , mabasi yanakimbia yanavyotaka wenye jukumu la kulinda usalama barabarani wanapiga porojo watu wanakufa utadhani ni msimu wa ajali.

Siku hizi hadi viongozi wa dini wamekumbwa na tabia ya kupiga porojo , badala ya kutetea wanyonge wao wanagombana wenyewe kwa wenyewe, wengine wanaenda mbali zaidi kwa kujigeuza miungu watu wanadanganya masikini na kuwakamua hata kidogo walichonacho na wengine wamejigeuza watabiri wanatabiria watu kufa? Hizi ni porojo tupu.

Sasa katika muktadha huu ndio maana najiuliza kuwa nchi hii iliyolewa kwa wingi wa porojo itaendelea vipi? Badala ya kwenda mbele sisi tunarudi nyuma kwasababu ya porojo zisizokwisha na hazina mipaka hata kwenye mambo ya msingi tunapiga porojo au ndio tunategemea kuendelea kwa miujiza ya Mussa? Tafakari!
Imeandikwa na:

Nova Kambota Mwanaharakati,
0717 709618 au +255717 709618
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa,
June 30, 2011

No comments:

Post a Comment