Na Ahadi Kakore
Mshambuliaji wa kutumainiwa wa Yanga, Davies Mwape atalazimika kupumzishwa kwa muda usiojulikana baada ya kuumia nyama za paja.
Yanga na Simba zinakutana Julai 17 katika mechi ya Ngao Hisani na daktari wa Jangwani, Juma Sufiani amesema hana uhakika kuhusiana na Mwape atarejea lini uwanjani.
Mwape raia wa Zambia aliumia paja la kulia kwenye mazoezi ya timu yake yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Kaunda jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano jana, Sufiani alisema: “Kwa sasa ni mapema kueleza lolote kwa sababu hadi nimuangalie na kufanya uchunguzi wa kina ndiyo nitakuwa katika wakati mzuri wa kuelezea tatizo lake,” alisema Sufiani, dakika chache baada ya Mwape kuumia.
“Hapa itakuwa hivi, vipimo ndiyo vitaonyesha arudi uwanjani baada ya muda gani. Inaweza kuwa hivi karibuni au baada ya muda mrefu, inategemea.”
Kuhusiana na kipa namba moja wa timu hiyo, Yaw Berko raia wa Ghana ambaye alivimba mwili mzima, Sufiani alisema:
“Lakini upande wa Berko bado anaendelea kufanyiwa uchunguzi ingawa ameshapona kwa kiwango cha kuridhisha na huenda kama vipimo vikionyesha hakuna tatizo kubwa ataanza mazoezi mepesi haraka iwezekanavyo.”
Awali Berko alikuwa akisumbuliwa na malaria lakini hivi karibuni alivimba mwili mzima baada ya kula kitu kisichojukana na dawa zake kuagizwa Ghana.
No comments:
Post a Comment