Mshambuliaji Kenneth Asamoah raia wa Ghana, jana alipeleka faraja kuu makao makuu ya klabu ya Yanga, Jangwani baada ya kufunga bao muhimu.
Bao hilo la Asamoah, liliwazima mashabiki lukuki wa Simba waliojitokeza kuishangilia timu yao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mghana huyo alifunga kwa kichwa katika dakika ya 109, baada ya kuunganisha krosi maridadi ya kiungo wa zamani wa Simba, Rashid Gumbo.
Yanga na Simba, zilishindwa kufungana katika dakika 90, zilipoongezwa dakika 30, Timbe akamuingiza Asamoah kuchukua nafasi ya Jerry Tegete baada ya kuwa amecheza dakika 15 za nyongeza hiyo.
Wakati Yanga wanajiandaa kupokea kombe, kilitokea kituko cha karne baada ya umeme kuzimika uwanjani hapo, hali iliyokuwa ikitishia usalama. Shughuli hiyo ilifanyika kwa kutumia mwanga wa gari la wagonjwa lenye namba za usajili STK 7374.
Ushindi huo unaifanya Yanga kubeba taji lake la kwanza la Kagame kwenye ardhi ya Tanzania Bara. Mara zote tatu, kombe hilo limetua Jangwani likitokea Uganda mara mbili na Zanzibar.
Huku mashabiki wakiwa wamejitokeza kwa wingi kwenye uwanja huo, mchezo huo ulikuwa wa vuta ni kuvute huku ukiwa umetawaliwa na vibweka vingi.
Katika moja ya wachezaji watakaokumbuka mechi ya jana, ni Mwinyi Kazimoto ambaye aliitumikia klabu yake hiyo mpya dakika 16 kisha kutolewa nje baada ya kuumia baada ya kuumizwa na Juma Seif ‘Kijiko’.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kuanzia saa 8 mchana, mabingwa wa Sudan, El Mereikh waliifunga St Georges ya Ethiopia kwa mabao 2-0 huku ngome ya Wahabeshi ikionekana kuwa na makosa mfululizo.
Vikosi viliundwa hivi, Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Godfrey Taita, Nurdin Bakari, Jerry Tegete, Davies Mwape na Hamis Kiiza.
Kikosi cha Simba kiliundwa na Juma Kaseja, Said Nassor ‘Chollo’, Amir Maftah, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Patrick Mafisango, Shija Mkina, Mwinyi Kazimoto, Mussa Hassan Mgosi, Haruna Moshi ‘Boban’ na Ulimboka Mwakingwe.
Wakati huo huo, mashabiki wa Yanga walikuwa wakilalamika mara baada ya umeme kukatika huku wakisema ni kitendo cha aibu kwa timu kukabidhiwa kombe katika hali kama hiyo.
Mashabiki hao ambao wengi wao walikuwa wakitumia mwanga wa simu zao walikuwa wakitoka nje huku wakilalama na kupiga kelele kutokana na kitendo hicho.
Aidha, shabiki mmoja wa Yanga ambaye jina lake halikupatikana alianguka na kuzimia wakati mchezo ukiendelea kutokana na kile kilichoelezwa kuwa na presha ya mchezo, alichukuliwa na watu wa huduma ya kwanza ‘red cross’ waliokuwepo uwanjani hapo na kupatiwa huduma ya kwanza.
SOURCE: GPL
No comments:
Post a Comment