Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo amesimamishwa kazi, lakini ataendelea kupokea malipo, huku akipisha uchunguzi ufanyike kuhusu kashifa ya barua aliyoiandika kwa idara mbalimbali za Wizara hiyo, akitaka mchango wa kiasi cha fedha za Kitanzania milioni 50 ambazo zingetumika kuwashawishi Wabunge wapitishe bajeti ya Wizara yake.
Tuhuma hizo na taarifa ya kusimamishwa huko imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, mbele ya waandishi wa habari huko Dodoma ambaye aliongeza kuwa tuhuma nyingine zinayomkabili Jairo ni zile za kuwalipa masurufu ya safari watumishi walio chini ya Wizara na Taasisi zake ambao tayari walishalipwa na Wizara na taasisi zao.
Utekelezaji wa taarifa hiyo unaanza rasmi kesho.
Luhanjo alisema akiwa ndiye mwenye Mamlaka ya Nidhamu, kwa kuwa tuhuma zinazomhusu Jairo zinahusu fedha, amemteua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kumpa siku 10 afanye uchunguzi wa awali. Ndani ya siku 2 - 3 atakuwa amemteua Kaimu wa nafasi hiyo wakati Jairo akiwa likizo ya malipo. “Siku mbili, tatu mtasikia nani nimemteua,” alisema Luhanjo.
Luhanjo alisema kwa kuwa tuhuma zinazomhusu Jairo ni nzito, imemlazimu kuamua aende likizo licha ya kwamba Sheria Na. 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma 2003, inaruhusu mtuhumiwa kuruhusiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi unafanyika.
source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/07/david-jairo-asimamishwa-kazi-kupisha-uchunguzi.html#ixzz1Sohp7l00
No comments:
Post a Comment