Wanafunzi wawili wa darasa la saba katika shule ya msingi Kidugalo wilayani Morogoro, wamehukumiwa adhabu ya kuchapwa viboko sita kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi mwenzao.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Jafari Mzonge wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo. Wanafunzi hao, Salama Said (14) na Shaaban Kefa (14), walimlawiti mwanafunzi mwenzao wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 12 na kumsababishaia maumivu.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mzonge alisema ametoa adhabu hiyo kali kwa watoto hao baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka.
Hakimu Mzonge pia alisema amefikia uamuzi huo wa kutoa adhabu ya viboko kwa kuzingatia kwamba wanafunzi hao bado watoto na ni kosa lao la kwanza.
Awali, akisoma maelezo ya kosa, Mwendesha Mashitaka Salehe Kalulu, alidai kuwa washitakiwa walitenda kosa Novemba 26, mwaka jana, saa 12.30 jioni, katika kijiji cha Kidugalo, Ngerengere.
Hata hivyo, alidai kuwa adhabu iliyotolewa kwa wanafunzi hao ni ya kuridhisha kutokana na umri mdogo walionao na hivyo si vyema kuhukumiwa kifungo ikizingatiwa ni kosa lao la kwanza.
Alidai pia hukumu hiyo itakuwa fundisho kwa wanafunzi wengine wenye tabia kama hiyo na kuwaonya kutoendelea na vitendo hivyo.
source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/06/wanafunzi-2-wachapwa-kwa-kumlawiti-mwenzao.html#ixzz1PY0uAAij
No comments:
Post a Comment