TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Msingi wa Maendeleo ni Haki.
“Ninawasalimu wote .
Hivi karibuni, tarehe 21 Juni 2011 siku ya jumatano kuna taarifa nyingi
ziliandikwa katika vyombo vya habari kuhusu muafaka dhidi ya mgogoro
wa uchaguzi wa umeya uliokuwa unaendelea hapa mjini Arusha .
Ni kweli kabisa mgogoro wowote humalizwa kwa vikao na mashauriano, na
ndivyo ambavyo CHADEMA tumekuwa tukitaka toka awali na mimi binafsi
natamani tukae kwa amani katika nchi yenye misingi ya haki na utawala
wa kuzingatia sheria. Kimsingi kabisa tulitaka serikali ya CCM itamke
kuwa kosa limefanyika kwa kutozingatia kanuni ya uchaguzi wa umeya wa
Arusha na kupelekea hapa tulipofika.
Mchakato wa muafaka ulipoanza mwanzoni mwa mwezi APRILI 2011 ulikuwa
na nia ya kuitaka serikali ione makosa hayo na ichukue hatua kwa
wahusika waliosababisha kufika katika hali tata tuliyofikia sasa na
sio kufarijiana kwa vyeo. Mgawanyo wa nafasi au vyeo ni mapendekezo tu
yenye kutaka madiwani wote kushiriki utumishi kwa wananchi lakini
haikuwa msingi wa madai yetu.
Baada ya kufanya utafiti na kufikiria kwa makini juu ya mchakato wa
kufikia muafaka huu ndipo nilipogundua pamoja na nia nzuri ya CHADEMA,
serikali ya CCM haijachukulia kwa nia na dhati ya kweli ili kutoa
majibu ya msingi ya madai yetu kuhusu HAKI na KUZINGATIA KANUNI lakini
pia kuonyesha toba na ukiri wa makosa yaliyofanyika ili wananchi
waweze kutuelewa.
Kwa sababu ya muafaka huu kushindwa kutoa majibu ya msingi kwa kweli
siwezi kukaa kimya hata kidogo juu ya muafaka huu ambao ni
udhalilishaji wa utu wa Mwanadamu na haki kwa kiwango cha hali ya juu
sana na katika mambo ya msingi tuliyokuwa tunapinga katika suala la
umeya ni ukiukwaji wa haki , taratibu na sheria katika uchaguzi wa
umeya uilokuwa umefanyika Arusha Mjini pamoja na sababu nyingine hii
ilikuwa ni sababu ya msingi ya kupinga jambo hili hata tukaamua
kufanya maandamano tarehe 5/1/2011 yaliyopelekea watu watatu kuuwawa
kikatili na polisi na wengine zaidi ya 26 kuhumizwa vibaya huku
wakiachwa na vilema vya maisha.
Hatukupinga utaratibu huo ili tugawane vyeo na nafasi mbali mbali
katika manisipaa ya Arusha hili halikuwa lengo letu na kamwe haliwezi
kuwa lengo langu .
Hatukuwa tunampinga Meya wa Arusha kwa dini yake au kabila lake au
rangi yake tulipinga mfumo uliomchagua ambao ulikiuka utaratibu wa
msingi wa kanuni na sheria za uchaguzi pamoja na mambo mengi
yaliyohusu haki na usawa ,ukweli .
Tulisema Ocd wa Arusha aondolewe na polisi washitakiwe juu ya mauwaji
ya watu wasio na hatia na familia zao zilipwe fidia.
Tulitaka mkurugenzi wa manisipa ya Arusha aondolewe kazini kwa
kusimamia uchaguzi batili nakusababisha majonzi mengi na vifo vya raia
wasio na hatia.
Tulitaka uchaguzi wa umeya urudiwe hapa mjini Arusha na haki itendeke
na sio kugawana uongozi na mambo mengi ya msingi ambayo kila mtu
anajua na hata ulimwengu mzima unajua.
Hivyo basi siwezi kukubali dhambi hii na udhalimu huu eti tu kwa
sababu chadema imepewa unaibu meya kwani huu sio msingi mama wa
muafaka na kama suala ni unaibu Meya mbona tulimuona Diwani wa kata ya
Sokoni one Mh Kivuyo kuwa ni msaliti alipokuwa ni naibu Meya ?
Ninatambua na ninajua inaweza kuwa vigumu kueleweka katika hili au
kupewa tafsiri nyingi nyingi tu, napenda kujiweka wazi kuwa
nitasimamia ukweli daima kwa maslahi ya wananchi na niko tayari
kusimama na wananchi kukabiliana na upinzani wowote ili kuwatetea
maana mimi ni mtumishi wao kwani Haki na utu sio jambo la kupuuza na
kujadiliwa kwa vyeo au pesa.
Mwisho naomba mwenyezi Mungu anisaidie na watu wote wa Arusha mjini na
watambue mgogoro hauwezi kuzuia maendeleo ya Arusha Mjini hata kidogo
kwani hata bajeti ya 2011 -2012 ilipitishwa bila hata kuzingatia
kanuni na taratibu. Kuna wafanyabiashara wachahe wa Arusha
wanaoshawishiwa kuwa Haki hii tunayoitafuta inadumaza ukuaji wa
biashara zao, napenda kuwaambia kuwa Mgao wa Umeme, Ufisadi, Rushwa,
uonevu, kutokufutwa kwa kanuni na Ulaghai wa Serikali iliyopo
madarakani ndivyo vinavyodumaza uchumi wa Taifa na Chadema inapambana
ili kuhakikisha inajengwa Tanzania Mpya yenye kufuata Kanuni na
utaratibu na mfumo wa sheria utakaoleta Neema ya kweli Tanzania.
Ni nayo ilani yangu kwa wananchi wa Arusha nitatimiza kwa mipango yangu
na yale ya kisera yanayohusu Nchi nitaendelea kuongea kwa nguvu zote
kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutumia vyombo
vingine kama Mbunge.
Na pia niwaombe Madiwani Wafikirie kwa makini utashi wenu dhidi ya
jambo hili nimatumaini yangu mtakuwa mlifanya maamuzi kwa haraka sana
bila kiuzingatia ukweli.
Arusha nawaomba sana na mnapaswa kuwa wavumilivu na majasiri wakati
huu ambapo tunapita katika majaribu mengi katika kupigania
ukweli ,hatuwezi kuudhalisha utu wa mwanadamu na haki kwa kugawana
vyeo kwa kisingizio cha maendeleo, Hata hivyo hakuna maendeleo Duniani
yanayopita haki ,ukweli , utu , usawa ,na kama kuna mtu yeyote
anafikiri anaipenda Nchi yake basi awe mfano wa kufikiria na kutenda
Haki .
Msiogope Mungu yuko pamoja nasi Ukweli utashinda. Mungu Awabariki
sana.
GODBLESS J LEMA ( Mbunge Arusha Mjini )
…………………..........
27/6/2011.
No comments:
Post a Comment