KLABU ya Yanga imethibitisha kumalizana na kiungo mshambuliaji wa Uganda na Klabu ya Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam, Owen Kasule, kwa ajili ya kuichezea kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Awali, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, alikuwa akiwaniwa vikali na Simba ambao walifunga safari hadi Uganda kwenda kumsajili lakini wakagonga mwamba.
Kiungo huyo alipendekezwa na Hamis Kiiza asajiliwe Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa 2012/2013 kutokana na uwezo wake ndani ya uwanja.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmeid ‘Seif Magari’, ameliambia Championi Jumatano kuwa wameshamalizana na kiungo huyo ikiwa ni pamoja na kumpa fedha za usajili na kilichobaki ni kusaini mkataba tu.
Seif alisema kiungo huyo alitarajiwa kuwasili jana kwa ajili ya kusaini fomu ya usajili na kumalizia baadhi ya mambo mengine muhimu.
“Kasule tumeshamalizana naye, ikiwemo kumpa fedha za usajili, kilichobaki ni saini yake atakayosaini kesho Jumanne (jana) baada ya kutua nchini akitokea kwao Uganda.
“Tumefikia hatua ya kumsajili Kasule kutokana na upungufu uliopo kwenye safu ya ushambuliaji, tunaamini akiwemo yeye na Kiiza, watatusaidia,” alisema Seif.
Kiungo huyo mshambuliaji aliwahi kung’ara na timu za Uganda zikiwemo Bunamwaya na Kampala City Council.
Kasule ni mmoja wa viungo bora kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda ambayo pia anaichezea mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, na wote wamekuwa wakianza katika kikosi cha kwanza.
Na Wilbert Molandi, GPL
No comments:
Post a Comment