UONGOZI wa Yanga umefumba macho na kuwakata wachezaji watano wa timu hiyo akiwemo aliyekuwa nahodha, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’.
Yanga kwa sasa ipo kwenye presha kubwa ya kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia kumaliza ligi ya msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya tatu na kukosa tiketi ya kushiriki michuano yoyote ya kimataifa.
Kwa mujibu wa chanzo muhimu kilicho ndani ya klabu hiyo, mbali na Nsajigwa, nyota wengine waliotupiwa virago vyao ni pamoja na Kenneth Asamoah, Davies Mwape, Chacha Marwa, Zubery Ubwa na Amour Atiff.
Chanzo hicho ambacho hakikupenda kutajwa jina kilisema kikosi hicho kwa sasa kimebaki na nyota 22 tu huku mchujo huo ukitarajiwa kuendelea mpaka watakapobaki 16, kabla ya kuanza kusajili wengine.
“Uongozi umejipanga kuhakikisha klabu inasukwa upya kwa usajili mkali, hivi ninavyoongea na wewe tumetoka katika kikao kizito na tumewakata nyota watano akiwemo Nsajigwa.
“Wiki ijayo (wiki hii) kutakuwa na kikao kingine ambacho kuna uwezekano kati ya hao 22 wakakatwa wengine sita,” kilisema chanzo hicho.
Majina ya wachezaji waliobaki Yanga ni makipa; Shaban Kado, Yaw Berko na Said Mohamed ,wakati mabeki ni; Salum Telela, Ibrahim Job, Oscar Joshua, Stephano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Abuu Ubwa na Godfrey Taita.
Viungo ni Nurdin Bakari, Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif, Haruna Niyonzima, Rashid Gumbo, Idrisa Rashid, Shamte Ally na Godfrey Bonny huku washambuliaji wakiwa ni Jerry Tegete, Hamis Kiiza, Kigi Makasi na Pius Kisambale.
Na Khatimu Naheka
No comments:
Post a Comment