KLABU ya Simba imeamua kujiimarisha zaidi kwa kumrudisha kundini kiungo mshambuliaji wake wa zamani, Daniel Mwarwanda ‘Mrwanda’ kwa ajili ya msimu ujao.
Mrwanda ambaye alikuwa akiichezea DT Long ya Vietnam amekubali kurejea kuichezea Simba na tayari mazungumzo yapo katika hatua za mwisho na kama mambo yangeenda vizuri, huenda jana angesaini Msimbazi.
Mrwanda ambaye aliwahi kuichezea Simba kwa misimu miwili akitokea AFC Arusha kabla ya kutimkia Kuwait katika Klabu ya Al Tadamoun akiwa na Nizar Khalfan, amesema yupo tayari kurejea nyumbani.
“Mrwanda amekubali kuichezea Simba, tunaamini atakuwa msaada mkubwa kutokana na uzoefu wake hasa katika michuano ya kimataifa,” chanzo cha uhakika kililieza Championi Jumatatu.
“Unajua kocha (Milovan) alikuwa anataka kiungo wa pembeni, kwa wachezaji walio hapa nyumbani aliona (Mrisho) Ngassa ndiye chaguo sahihi, lakini inaonekana kama Azam FC hawataki.
“Hivyo Mrwanda anaweza kuwa chaguo zuri, tunajua atatusaidia na kizuri mwenyewe ameonyesha nia ya kuichezea Simba. Ni kijana wetu na atakuwa amerudi nyumbani.”
Kuhusiana na hilo, Mrwanda akizungumza jana mchana jijini Dar es Salaam alisema: “Kuna mazungumzo yameanza kati yangu na Simba, kama mambo yatakamilika basi nitatoa taarifa rasmi.”
Milovan, raia wa Serbia, amesisitiza kutaka mshambuliaji mpya wa pembeni na kama Simba watafanikiwa kumnasa Mrwanda, maana yake Emmanuel Okwi atacheza pembeni kushoto, Mrwanda kulia wakati Felix Sunzu na Haruna Moshi ‘Boban’ watakuwa katikati.
Na Saleh Ally, GPL
No comments:
Post a Comment