BENDI Kongwe zenye upinzani wa jadi katika muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park, zimepangwa kupambana katika tamasha la maadhimisho ya miaka 5 ya klabu ya burudani ya Villa Park Resort ya jijini Mwanza.
KLABU ya Villa Park Resort ya Jijini Mwanza, itazipambanisha bendi kongwe za muziki wa dansi nchini , Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park.
Bendi hizo zinatarajiwa kupanda jukwaani Ijumaa kwenye uwanja wa CCM Kirumba, katika sherehe za kutimiza miaka 5 ya klabu hiyo ya burudani katika jiji la miamba ya mawe ‘Rock City’.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Villa Park, Shijani Mtunga, alisema sherehe hizo za miaka 5 zimelenga kufanya tathmini ya walikotoka na kuangaza mbele, kubwa ikiwa ni kurudisha fadhila kwa wadau wa klabu hiyo ambayo imekuwa ikitoa burudani za muziki kutoka kwa wasanii wa vikundi na bendi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, vinywaji na vyakula.
Alisema mbali na bendi hizo za Sikinde na Msondo, pia bendi ya Super Kamanyola wakiongozwa na Mukuna Roy, Lufungula Lulembo ‘Parash’,BennoVilla Antony na Ali Yahaya, itashiriki katika tamasha hiilo kama wenyeji.
Mtunga alisema bendi hizo zimethibitisha kushiriki na zitafanya maonyesho yao siku za Ijumaa na Jumamosi na kuhitimisha Jumapili wakisindiikizwa na Super Kamanyola.
Msanii Jokha Kassimu au Kanga Moko, yeye atakata utepe wa sherehe hizo kwa kupanda jukwaani Alhamis ili kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki wa mwambao 'Taarabu', huku Madj PQ , Dj John, Dj Chriss na Dj Mafuvu wakiwarusha wapenzi wa ngoma za kuruka na majoka (disco).
Meneja huyo alisema katika sherehe hizo kutakuwa na muziki pamoja na mchezo wa soka ikishirikisha majirani wa klabu hiyo wanaofanya nao biashara ya aina moja, klabu za Victoria, Shouters Pub na La Kairo. Burudani zote zitakuwa zikifanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Na Mashaka Baltazar, MWANZA
No comments:
Post a Comment