Thursday, June 7, 2012

Kutolewa kwa DKB na Zainab BBA, kumemuongeza Prezzo nafasi ya kuichukua $ 300,000


Waswahili wanasema ‘kufa kufaana’. Juzi DKB mwakilishi kutoka Ghana na Zainab mwakilishi kutoka Sierra Leone wametimuliwa kutoka kwenye Big Brother Africa Stargame baada ya kuvunja miongoni mwa sheria za Big Brother Africa kwa kupigana.

Mwanamitindo huyo wa Sierra Leone na mchekeshaji wa Ghana walijikuta katika mabishano mazito yaliyopelekea DKB kumtandika kibao kikali Zainab.

Kitendo hicho kilivunja sheria inayosema ‘Housemate yoyote atakayeonesha vitendo vya kikatili ataondolewa kwenye jumba hilo mapema iwezekanavyo’

Hata hivyo kutolewa kwa Zainab na DKB kwenye mashindano hayo kuna faida kubwa na hasara kidogo kwa mwakilishi wa Kenya Prezzo.

Hasara ni kuondoka kwa Zainab ambaye walitokea kuwa karibu kiasi cha kulitoa doa ‘penzi la runingani’ la Prezzo na Goldie. Prezzo na Zainab walitokea kuwa karibu zaidi kiasi ambacho kitamuumiza Prezzo kwa kukosa kampani.

Faida ni kuwa wote DKB na Zainab walikuwa miongoni mwa washiriki tishio kwa Prezzo katika msako wake wa kitita cha dola laki tatu zitakazotolewa kwa mshindi.

Kwa mujibu wa mahojiano ya mwanamuziki Mampi Mukate wa Zambia aliyetolewa kwenye mashindano hayo na gazeti la NewsDay la Zambia, mwanadada huyo mwenye miaka 25 alisema anaamini zawadi itamwendea Roki ama Zainab. Hivyo kuondoka kwa Zainab kunakuwa kumepunguza idadi ya washiriki tishio kwa Prezzo.

Kwa upande mwingine DKB, mchekeshaji mahiri nchini Ghana, uwepo wake ulikuwa tishio pia kwa Prezzo. Ikumbukwe pia mafahari hao nao ilikuwa kidogo ‘wazichape’.

Ukaribu wa Ghana na Nigeria ulikuwa unamfanya DKB awe na mashabiki wengi kwenye nchi hizo na hivyo kuwa kwenye orodha ya washiriki wa kuangalia sana.

Na sasa washiriki tishio kwa Prezzo waliosalia Upville ni Maneta na Rocki wa Zimbabwe, Barbz wa South Africa na Goldie wa Nigeria.

Juzi Keitta aliongezeka Upville baada ya mpenzi wake Eazzy ‘Mildred’ na kinadada ndugu Eve na Edith kutoka.

Hata hivyo mambo ndo kama yameanza kwakuwa shindano hilo halijamaliza hata siku 30 kati ya 90 watakazokaa washiriki kwenye jumba hilo. Mambo yanaweza kubadilika kadri siku zinavyokwenda. Yetu macho na masikio.

Source: Bongo 5

No comments:

Post a Comment