Monday, June 4, 2012

Kocha wa Ivory Coast aishangaa Taifa Stars


LIKIWA ni pambano lake la kwanza la ushindani tangu apewe timu, kocha wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Sabri Lamouchi ameshangazwa na kiwango kizuri cha wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika pambano la juzi dhidi ya timu yake.

Lamouchi ambaye anapingwa na baadhi ya mashabiki wa soka nchini hapa ambao wanaamini ana kiwango kidogo cha kuifundisha Ivory Coast, alisema hakutegemea kama Stars wangeweza kumiliki mpira kwa kiasi alichoona.

“Wametupa shida sana na nimeshangazwa kwa sababu sikutegemea kuona Tanzania ikicheza mpira huu. Walipoupata mpira hawakuupoteza kiurahisi hali iliyowalazimisha wachezaji wangu waingie katika mtihani wa kukaba pia,” alisema Lamouchi
kwa lugha ya Kifaransa huku akitafsiriwa na Solomoni Kalou ambaye alikuwa mkalimani wake kwa lugha ya Kiingereza.

“Stars ni timu nzuri, lakini naona wanakosa uzoefu kwa kiasi fulani, kama wakiendelezwa hivi kwa muda mrefu basi watakuwa na timu yenye ushindani kwa kiasi kikubwa na kundi hili litakuwa gumu,” alisema Lamouchi.

Naye Kalou ambaye alifuatana na Lamouchi katika mkutano huo wa waandishi wa habari alieleza kushangazwa kwake na kiwango cha Stars, lakini alisema alijua mechi itakuwa ngumu kwao.

“Tulijiandaa mapema kwa sababu tulijua mechi kama hizi zinakuwa ngumu. Tanzania walimiliki vizuri mpira na wakatupa wakati mgumu,” alisema kalou.

No comments:

Post a Comment