MSAFARA wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, uliwasili mjini Khartoum, juzi saa 5: 49 usiku na kukutana na mambo ya vituko kama yale waliyokumbana nayo kwa Waarabu wa Algeria, ES Setif.
Baada ya kutua katika uwanja wa ndege na mambo yote kukamilika, Simba walijikuta kwenye hali ya sintofahamu kutokana na kuwekwa uwanjani hapo bila sababu za msingi kwa zaidi ya saa moja na nusu.
Hali hiyo iliwaudhi maofisa wa Simba ambao walijaribu kuwasiliana na waliokwenda kuwapokea, maofisa wa Chama cha Soka Sudan (SFA).
Kama haitoshi, vituko viliendelea jana asubuhi Simba walilazimika kukaa nje kuanzia saa 4 asubuhi hadi 10 wakiwasubiri wenyeji wao waliodai walichelewa kwenye foleni ya barabarani.
Walikula chakula cha mchana saa 10 jioni na kuanza kujiandaa na safari ya kwenda Shandi, maana yake jana ambayo ingekuwa ni siku ya pili bila kufanya mazoezi.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, ameliambia Championi Ijumaa kuwa baada ya kuwasiliana na watu wa SFA, waliahidi kurekebisha mambo lakini wakajibu kwa jeuri kuwa wanalipa kisasi.
“Kiongozi mmoja wa SFA alisema hata kwetu tuliwafanyia hivyo, kitu ambacho hakikuwa sahihi. Wao walifika asubuhi na kila kitu kilikwenda vizuri.
“Zaidi ya saa saba na nusu (usiku) ndiyo tuliondoka uwanjani hapo. Bado tumewasubiri kwa saa sita pale hoteli baada ya kuwa tumeachia vyumba. Wanajaribu kutuchanganya,” alisema Kamwaga.
Simba iliwahi kufanyiwa vituko kama hivyo nchini Algeria ilipokwenda kucheza na ES Setif.
Wekundu hao wapo nchini humo kwa ajili ya kuvaana na Al Ahli Shandi kwenye mchezo wa pili wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho. Katika mechi ya kwanza, Simba iliwalaza Wasudani hao kwa mabao 3-0, hali inayowafanya wajaribu mbinu za ndani na nje ya uwanja ili kuwango’a vijana hao wa kocha, Milovan Cirkovic.
Kutokana na tukio hilo la ‘kugandishwa’ uwanja wa ndege, Milovan alisitisha mazoezi ya jana asubuhi lakini wakashindwa tena kufanya jana jioni kutokana na kuchelewa.
Baada ya ushindi wa 3-0, Dar, mechi hiyo ya marudiano itachezwa kesho Jumapili saa mbili usiku kwenye uwanja wa Shandi unaobeba mashabiki 10,000.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment