Monday, May 7, 2012

Taifa Stars yamstaafisha Poulsen


ALIYEKUWA kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen {pichani}, amesema kufuatia kusitishwa kwa kibarua chake cha kukinoa kikosi hicho, hatarajii kuwa kocha tena katika maisha yake.
Poulsen aliyedumu katika kikosi hicho kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, ajira yake ilisitishwa wiki chache zilizopita katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia wajumbe wengi wa mkutano huo kusema kuwa hawajaridhika na kiwango chake cha ufundishaji.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Poulsen, raia wa Denmark, alisema ameona ni vyema sasa akaachana na kazi ya ukocha ili aendelee na kazi zake binafsi, kutokana na umri wake wa miaka 56 kuwa mkubwa.

Alisema ingawa amekuwa akipata ofa nyingi katika nchi za Uarabuni, kwa sasa hawezi kufanya kazi hiyo kwa kuwa umri wake haumruhusu kuendelea kuwa kocha.

Poulsen ambaye mkataba wake ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu, ameshindwa kuwashawishi Watanzania kutokana na kikosi chake kutofanya vizuri katika mechi nyingi.

“Baada ya kukutana na rais (Leodegar Tenga) na kunitaarifu kwamba mkataba wangu hautaongezwa, nadhani kwa sasa imetosha na sitaweza kuwa kocha tena, ingawa nimekuwa nikipata ofa nyingi katika nchi za Uarabuni,” alisema Poulsen na kuongeza:
“Nawashukuru Watanzania wote kwa ushirikiano wote walionipa tangu mwanzo mpaka sasa lakini pia nimesikia kwamba Kim (Poulsen) anaweza akapewa majukumu Taifa Stars, ni mtu sahihi na namtakia kila la kheri na mara nitakaporudi kutoka Nigeria nitazungumza naye kabla ya kuondoka, kwa sababu ni rafiki yangu sana.”

Kim Poulsen ambaye pia ni raia wa Dernmark, inaelezwa kuwa, anaelekea kupewa majukumu ya kuinoa Taifa Stars kwa muda, kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa katika vikosi vya timu za taifa za vijana.

Jan Poulsen anaondoka Stars huku akiwa na kumbukumbu ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji linalohusisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.

GPL

No comments:

Post a Comment