SIKU chache baada ya Kim Poulsen kutangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, raia huyo wa Denmark ameibuka na kusema kuna uwezekano mkubwa kikosi hicho kikawa na viungo Haruna Moshi ‘Boban’ na Athuman Idd ‘Chuji’.
Poulsen ambaye alikuwa kocha wa kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, amepewa nafasi hiyo kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kumsitishia mkataba aliyekuwa kocha wa Stars, Jan Poulsen ambaye mkataba wake ulipaswa kufikia kikomo Julai, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Poulsen alisema amekuwa akiwafuatilia kwa makini nyota hao wawili na amebaini ni wachezaji wazuri ambao wameonyesha uhai katika michezo mbalimbali ya klabu zao kwa kujitolea kwa kiwango kikubwa ili timu zao zipate matokeo mazuri.
Alisema kuwa kwake yeye mchezaji anayejituma katika klabu yake ndiye atakayepata nafasi ya kuichezea Stars.
“Ninachoweza kusema kuhusu hilo ni kwamba, nimekuwa nikiwafuatilia mara kwa mara katika michezo mbalimbali ya timu zao na wamekuwa wakionyesha uhai mkubwa kwa kuhakikisha wanajituma vizuri katika klabu zao hatua ambayo kwa kocha yeyote atafurahia,” alisema Poulsen na kuongeza:
“Kwangu mimi kama unajituma vizuri katika klabu yako basi ni wazi unaweza kupata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa na kwa kuwa Jumatatu (leo), natakiwa kutangaza kikosi, nyota hao wana nafasi kubwa ya kuwepo lakini nadhani tunapaswa kusubiri mpaka Jumatatu (leo) ili tuone hilo.”
Poulsen anatarajia kuita kikosi cha Stars kwa ajili ya maandalizi ya mechi za mchujo wa Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast Juni pili nchini humo na dhidi ya Gambia Juni tisa jijini Dar.
Na Khatimu Naheka
No comments:
Post a Comment