Thursday, May 31, 2012

Mjadala wa nauli mpya za daladala ulivyoibua jazba


WAKATI wananchi wawakitembea kwenda kazini majira ya asubuhi na kurudi nyumbani jioni, mamlaka husika zimejadiliana kupandisha nauli kwa asilimia 150 kwa wakazi wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam.

Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), na Wamiliki wa daladala (Dacoboa) wamejadiliana kufanya mabadiliko hayo wiki iliyopita, katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam

Wakati wakifikiria kuongeza nauli, wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kumudu kiwango hicho kutokana na thamani ya shilingi kushuka baada ya kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni kuliko shilingi.

Kwa mfano, ukiwa barabara ya Morogoro, Kawawa au Uhuru; majira ya asubuhi utaona makundi ya watu katika maeneo ya Manzese, Magomeni, Kigogo, Ilala na Chang’ombe wilayani Temeke; vijana, wazee na wanafunzi wakitembea kwa kasi kuelekea kati kati ya jiji kutafuta riziki na wanafunzi wakielekea shuleni.

Wananchi wapinga nauli mpya
Pamoja na hayo wakati mjadala wa kuongeza nauli, ukifanyika katika ukumbi wa Karimjee, wiki iliyopita watu wengi hasa wa kawaida walikuwa na jazba kusikia kwamba nauli itaongezeka kutoka Sh350 ya sasa mpaka Sh870.

“Haiwezekani kulipa Sh870 wakati makondakta ni wachafu,” anasema mmoja wa watu waliudhuria mjadala huo.
Lakini wananchi kwaujumla, hawataki kabisa kusikia mjadala huo. Hawataki kusikia nauli inapanda mpaka Sh870!.
Wanapinga kwa sababu gharama za maisha ziko juu. Huduma za daladala ni mbovu pia, lakini kubwa zaidi mifuko yao haina fedha.

Mjadala huo ambao ulifanyika kwa zidi ya saa nne uligusa hisia za watu na kusema sekta ya usafiri inatoa huduma duni kwa abiria.

Licha ya kueleza hayo watumiaji wa usafiri walielezea kupinga ongezeko hilo kwa kubainisha sababu mbalimbali.

Wakichangia mjadala huo wakukusanyamaoni, wananchi wanashauri wapiga debe wasipewe fedha na badala zitumike kuziba pengo wanalolalamikia wamiliki wa daladala.

“Fedha nyingi wamekuwa wakizitupa barabarani kwa kuwapa wapiga debe, leo wanatuambia wanataka kuongeza nauli kwa nini wasingezuia wapiga debe ili fedha wanazowapa zisaidie kuongezea hizo gharama wanazodai kwamba zimepanda,”anaeleza Salum Abdallah

Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Hamisi Selemani anasema zitolewa na kampuni kwa kuwa watu binafsi wanajali zaidi maslahi.

Selemani anashauri Serikali iboreshe miundombinu ili wamiliki wasitumie ubovu wa barabara kama kigezo cha kuongeza nauli.

Naye Aisha Mohamedi mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisutu anasema nauli isiongezwe kwa sababu na kwamba imeki ya Sh150.

“Tumekuwa tunapata usumbufu mkubwa licha yakulipa nauli ya Sh150, sasa kama wanataka kuongeza nauli huku tukiwa hatupati haki kama abiria wengine bado itakuwa kikwazo kwetu,”anasema Mohamed.

Husen Ally alieleza kwamba hapa awali nauli ya mwanafunzi ilikuwa Sh50, lakini ilizidi kupanda mpaka kufikia Sh150 jambo ambalo kwa sasa ni mzigo kwa wazazi kutokana na hali ngumu ya maisha iliyopo sasa.

“Kiukweli tunaomba mapendekezo hayo yasituguse kwani sisi tunategemea wazazi ambao nao vipato vyao ni vidogo na kama itashindikana Serikali ilete magari maalumu ya wanafunzi,” anasema Ally

Mbali na madereva na makondaktakwa kuwapa wapiga debe,pia wanalalamikiwa kwa kuzidisha viwango vya nauli majira ya usiku, kukatisha ruti, na kutumia lugha chafu kwa abiria.

Tacoboa: Tunapendeleza nauli mpya
Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Dacoboa), wakiwasilisha mapendekezo na sababu za kupandisha nauli kutoka Sh350 mpaka Sh870, wanasema wanalazimika kufanya hivyo kwa sababu gharama za undeshaji zikojuusasa.

Mwenyekiti wa Dacoboa, Sabri Mabruki anaeleza kwamba gharama za maisha zimepanda na kusababisha shughuli za uendeshaji wa biashara hiyo kuwa juu.

Anasema licha ya kutoza nauli ya Sh350, bado wamekuwa wakibeba askari bure na kuwatoza wanafunzi Sh100, jambo ambalo kwake anaona wanabebeshwa mzigo ambao siyo wakwao.

“Gharama za undeshaji wa biashara hii ya usafiri zipo juu, lakini bado tunafanya biashara katika miundo mbinu mibovu ya barabara.

“Tumekuwa tukiwa wabeba askari bure pamoja na wanafunzi kwa kuwatoza nauli ya Sh100, mzigo tunabebeshwa na Serikali jambo ambalo sisi kama wafanyabishara tunaona siyo jukumu letu,”anasema Mabruki.

Sumatra:Sisi ni wasikilizaji tu
Kaimu Mwenyekiti wa Sumatra Ahmad Kilima anasema kazi yao ni kusikiliza na kupitia mapendekezo hayo, lakini wadau wa usafiri ndiyo wenye uamuzi wa kukubali au kukataa.

Kwa upande mwingine anasema kwamba ni vyema wasafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam wakaanzisha kampuni ya usafiri ili Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart), utakapoanza uweze kutoa nafasi nzuri ya kuwashirikiasha na kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi.

Katibu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumtara CCC), Raurence Simo anasema hivi sasa siyo wakati mwafaka kwa wamiliki wa daladala kuongeza nauli kwa sababu mazingira ya kutoa huduma ya usafiri, hayajaboreshwa.

Huduma ya usafirishaji wa abiria katika Jiji la Dar es Salaam, zinatolewa chini ya viwango kwa kuwa madereva na makondakta, hawana ujuzi wa kazi hiyo.

Simo anasema kabla ya kuwapo kwa vyombo binafsi vya usafiri kulikuwapo na Shirika la Usafiri (DMT), na mwaka 1974 lilitaifishwa na kuwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), na baada ya UDA kulemewa, wasafirishaji binafsi (Daladala), waliruhusiwa kuendesha bishara hiyo.

“Leo asilimia 99 ya uduma ya usafiri wa umma inatolewa na daladala jijini Dar es Salaam na sekta hiyo imejaa msongamano, vurugu na fujo kutokana na kukosekana kwa usimamizi wa kitaalamu, sheria na kanuni za usafirishaji,” anabainisha Simo.

Simo anaeleza kwamba kutokana nasababu hizo nauli haziwezi kupandishwa.

Kwa upande mwingine bado kuna matatizo makubwa katika uendeshaji wa biashara hiyo natakwimu zinaonyesha kwamba malalamiko ya abiria katika suala la nauli linafikia asilimia 50 hasa majira ya jioni wakati makondakta wanapopandisha nauli.

Matatizo ya kukatisha rutini asilimia 21, lugha chafu zinazotolewa na makondakta na madereva kwa abiria ni asilimia 29, jambo ambalo ni kigezo kikubwa kwa wananchi kupinga ongezeko hilo.

Kauli za madereva
Lakini suala hilo pia liligusa hisia za wafanyakazi wa vyombo vya usafiri na Katibu wa Umoja wa Madereva wa Tanzania, Salmu Abdallah anasema wamiliki wa daladala hawapaswi kuomba kuongezewa nauli, kwa sababu hawana mikataba ya kazi.

Anasema ongezeko la nauli, litazidi kuwanyima watendaji hao haki zao na kuwafaidisha wamiliki wa vyombo vya usafiri.

“Mikataba ya kazi ambayo inawasilishwa Sumatra na wamiliki hao ni bandia, wanatumiamikataba bandia kupata vibali vya kuendesha biashara zao za usafirishaji na siyo vinginevyo” anasema Abdallah.

Takwimu zinaonyesha kwamba ongezeko la nauli limekuwa likifanyika kila mwaka.
Itakumbukwa wazi kwamba mwaka 1980, kulikuwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam nanauli ilikuwa Sh30, lakini ilipofika mwaka 1980 hadi mwaka 1990 UDA, walipandisha nauli mpaka kufikia Sh100.

Lakini haikuishia hapona mwaka 1990 mpaka 1995, nauli iliongezeka na kufikia Sh150, kutoka Sh100.

Mabadiliko hayo yaliendelea kutokea licha ya bei ya mafuta; dizeli, petroli na mafuta kuwa chini tofauti na sasa,lita moja ya petroliinauzwa Sh2,144.

Mwaka 1995, mpaka kufikia mwaka 2,000, nauli ilizidi kupanda mpaka kufikia 250, lakini haikuishia hapo kwani mwaka 2,000 mpaka mwaka huu, nauli imeongezeka na kufikia Sh300, kwa njia fupi, Sh 350 kwa ruti ya kati na Sh 500, kwa ruti ndefu jambo ambalo bado ni kero kwa wananchi.

Lakini sasa wamiliki wa daladala wanafikiria kuongeza nauli kwa zaidi ya asilimia 150. Kutoka Sh350 mpaka ,kufikia Sh870.

Ukweli ni kwamba bado sekta ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam bado upo nyuma kwani kumekuwa namatatizo makubwa kutokana na mamlaka za usafiri wa daladala kutokuwa makini.

Pamoja na kwamba Dacoboa, wanasema kwamba wataboresha huduma za usafiri, wanatakiwa kutumia busara katika mpango wao wa kuongeza nauli ili wasiwaumize wananchi.

Na Aidan Mhando, Mwananchi

No comments:

Post a Comment