Thursday, May 31, 2012

Milovan agoma kusaini Simba


KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amegoma kusaini mkataba mpya na klabu yake hiyo.

Milovan, raia wa Serbia, anataka kuongezewa maslahi zaidi ya yale yaliyopo kwenye mkataba wake wa awali.

Habari za uhakika ambazo Championi Jumatano limezipata, zinasema Milovan ameondoka nchini wiki iliyopita bila ya kusaini mkataba hadi uongozi huo utakapomuongezea maslahi zaidi.

“Kocha anataka mambo kadhaa, anataka aongezewe maslahi lakini pamoja na tiketi kwa ajili ya mkewe ili awe anakuja kumsalimia hapa Tanzania angalau mara moja kwa mwaka na gari la kutembelea,” kilieleza chanzo cha uhakika.

Msisitizo unaonekana pia ni katika suala la kocha huyo kutaka kuongezewa mshahara wake na taarifa zinasema katika mkataba uliokwisha, alikuwa analamba dola 6,000 (zaidi ya Sh milioni 9), kwa mwezi.
Alipozungumzia kuhusiana na suala hilo jana mchana akiwa kwao Serbia, Milovan alithibitisha kweli hajasaini mkataba mpya na Simba.

“Bado kuna mambo ya kurekebisha, wakimaliza haina shida nitasaini. Kama itashindikana, nitaangalia kitu kingine cha kufanya,” alisema.

Kwa upande wa Simba, Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema: “Tutamalizana naye ndani ya siku chache baada ya makubaliano kufikiwa.”

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za Milovan ambaye ni pacha wa Milan Cirkovic, kupata ofa kutoka Uarabuni, hivyo Simba inapaswa kuwa makini.

Mara ya kwanza alipotua kuifundisha Simba miaka mitano iliyopita, aliamua kuondoka kwa madai ya mshahara mdogo ukilinganisha na ule aliokuwa akilipwa Dusan Kondic aliyekuwa Yanga.

Na Saleh Ally, GPL

No comments:

Post a Comment