Wednesday, May 16, 2012

Caf yaifungia Al Ahli Shandi


UONGOZI wa Simba umekubali matokeo ya kufungwa na kutolewa na wapinzani wao Al Ahli Shandi ya Sudan, lakini wekundu hao wameacha hasara kubwa kwa Waarabu hao kwa kusababisha kufungiwa kuutumia uwanja wao.

Simba ilitolewa na Shandi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Jumapili iliyopita kwa mikwaju ya penalti 9-8, baada ya timu hizo kutoka sare ya jumla ya mabao 3-3.

Akizungumza na Championi Jumatano, mwenyekiti wa timu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema kufuatia matukio kadhaa ya hatari waliyofanyiwa kwenye mji huo, waliomba Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuuchunguza uwanja huo.

“Tulifanyiwa vitendo ambavyo siyo vya kawaida, lakini tuliripoti Caf, lakini kabla ya majibu makamishna waliokuja kwenye ule mchezo wametuambia kuwa kuna uwezekano uwanja huo ukafungiwa kwa matumizi ya michezo ya kimataifa.

“Hata mazingira yake hayaridhishi, mbali na sharti hilo kubwa pia Caf inaendelea kupitia ripoti mbalimbali za maafisa wake waliotumwa kusimamia mchezo huo na kuna uwezekano mkubwa wakaufungia uwanja ule kabisa, kwani hauna hadhi ya kimataifa na usalama wake ni mdogo, “Lakini hata kama kuna mchezo utachezwa kule timu zitakuwa zinafikia Khatoum na kwenda kwenye mchezo siku husika kwa kuwa mazingira hayaridhishi,” alisema Rage.

Na Khatimu Naheka, GPL

No comments:

Post a Comment