Thursday, May 31, 2012

AfDB yainufaisha Tanzania


BENKI ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) , wametoa dola 2.9 bilioni za Marekani katika mikopo na misaada 121 ya kuendeleza miradi ya maendeleo kwa Tanzania, hivyo kuifanya kuwa moja ya mataifa yanayonufaika zaidi na benki hiyo.

Imeelezwa kuwa, fedha hizo zimetolewa katika kufanikisha miradi ya Kilimo, Miundombinu,Nishati ya umeme, Maji na miradi mingine mbali mbali ya kijamii, ikiwamo inayounganisha nchi za Afrika ya Mashariki.

Taarifa ya iliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa benki hiyo(AfDB), unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Arusha(AICC), imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa ya benki hiyo mwaka 1971, Tanzania imekuwa ni mdau wake muhimu.

Benki hiyo imetoa mikopo katika miradi mikubwa ya kati ya mwaka 2011/12 pamoja na msaada wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Namanga nchini Tanzania hadi Arthi River nchini Kenya.

Barabara hiyo ya kiwango cha lami ambayo kwa sehemu kubwa imekamilika kutoka Arusha mjini hadi mpaka wa Namanga na kutoka Namanga hadi Arthi River ambapo Rais wa AfDB, Donald Kaberuka juzi, alisafiri kutumia barabara hiyo na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo.

Benki ya AfDB ina jumla wanachama 53 barani Afrika huku nchi nyingine wanachama zikitoka nje ya Afrika.

Nchi hizo ni pamoja na Argentina, Austria, Belgium, Brazil, Canada, China, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, India, Italia, Japan, Korea, Kuwait, Uholanzi, Norway, Ureno, Saudi Arabia,Uhispania, Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani.

Mussa Juma, Arusha

No comments:

Post a Comment