Thursday, February 16, 2012


HABARI za chini ya kapeti zinadai kuwa mume wa mcheza sinema mkali Bongo, Irene Uwoya, Hamad Ndikumana au Baba Krish ameitwa na ndugu zake waishio Rwanda ili kujadili mgogoro wa ndoa yake, lakini amegoma kuondoka bila mkewe.

Kwa mujibu wa mpashaji wetu, ndugu hao wamekuwa wakisoma migogoro ya ndoa yao kupitia magazeti na mitandao mbalimbali na wamekuwa wakiumizwa sana hivyo kumtaka Ndiku kwenda huko kuzungumzia tatizo hilo sanjari na kufanya mambo ya mila na desturi.

“Ndikumana ameitwa kwao Rwanda kwa ajili ya kukaa kifamilia waone jinsi gani wanaweza kuweka sawa mgogoro wa ndoa yake na Irene, lakini jamaa hataki, nasikia anasema katu hatanyanyua mguu Tanzania bila kuwa na mkewe, mama Krish,” kilisema chanzo hicho.

Wakati huo huo, Amani hivi karibuni lilifanya mahojiano ya saa moja na dakika kumi na saba na Ndikumana nyumbani kwake, Sinza-Madukani jijini Dar ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia suala la kurudi kwake Cyprus na baadaye akagusia ishu ya kwenda Rwanda alikoitwa.
Ndiku: “Mimi kama kuondoka Tanzania ningekuwa tayari tangu Januari 15, 2012, lakini nipo hapa kwa ajili ya kuweka ndoa yangu katika mazingira mazuri, ndiyo niondoke.

“Kwa sasa siwezi kuondoka na kumwacha mke wangu nyuma, lazima niondoke na familia yangu.”
Ndikumana aliongeza kuwa, wasiwasi wake mkubwa ni kuwa akiondoka Tanzania peke yake, wabaya wa ndoa yake watapata nafasi ya kuivuruga na hatimaye kuvunjika moja kwa moja.

“Nina wasiwasi nikisema niondoke bila Uwoya, wabaya wa ndoa yangu ndiyo watatumia nafasi hiyo kuivuruga moja kwa moja,” alisema Ndiku.

Kuhusu kuitwa Rwanda, baba Krish alisema habari hizo si za kweli, kwani kama ni mawasiliano na ndugu zake huwa anatumia njia ya simu.

Baada ya kuzungumza na baba Krish, Amani lilimpigia simu Uwoya ili kumuuliza kuhusu kuondoka na mumewe.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, nyota huyo wa sinema ya Oprah alisema:
“Nani aende Cyprus? Siendi na mtu kokote, kwanza kwa sasa nina mpango wa kwenda sehemu ambayo hakuna yeyote atakayepajua, si Ndikumana wala wazazi wangu.”

Hata hivyo, habari zilizotufikia wakati tunajiandaa kwenda mitamboni zilisema kuwa, msukuma kandanda huyo ameitwa nchini Rwanda kwa ajili ya mazungumzo ya awali ya kuichezea timu ya Rayon Sports ya nchini humo msimu huu, lakini jamaa amekataa kwenda.

Habari zinasema, Ndiku amekataa safari hiyo ili kuendelea kuweka sawa mambo yake ya ndoa hapa Tanzania ingawa mkewe ameshakanusha sababu hiyo na kusema anasubiri msimu mpya wa usajili wa Cyprus, Mei, mwaka huu.


Na Imelda Mtema, GPL

No comments:

Post a Comment