Wednesday, January 4, 2012

PAPIC ATEMA TISA YANGA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mserbia, Kosta Papic, ametaja wachezaji tisa wasiokuwepo kwenye programu yake huku Hamis Kiiza, Rashid Gumbo na kinda la Arsenal, Amour Atiff, wakitajwa.

Yanga hivi sasa inashiriki Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar lakini imepeleka kikosi cha vijana katika michuano hiyo pamoja na wachache kutoka timu A, chini ya makocha, Fred Felix Minziro na Abubakar Salum ‘Sure Boy’.

Kikosi cha kwanza cha Yanga kimebaki jijini Dar es Salaam kikiendelea na mazoezi chini ya Kocha Mkuu, Kosta Papic, kikijiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara utakaoanza Januari 21, mwaka huu.

Kwa mujibu wa chanzo chetu makini cha habari ndani ya benchi la ufundi la Yanga, wachezaji wa timu A, walioongozana na Minziro pamoja na Sure Boy kwenda Zanzibar, hawapo kwenye mipango ya Papic kwa msimu huu.

Wachezaji hao wanatajwa kuwa ni Oscar Joshua, Zuber Ubwa, Said Mohamed, Idrisa Rashid ‘Messi’, Salum Telela, Ibrahim Job, Atiff, Gumbo na Kiiza.

“Wachezaji 20 waliobaki Dar es Salaam ndiyo Papic ana mpango nao katika mzunguko wa pili na Klabu Bingwa Afrika. Kocha mwenyewe leo (juzi) ameelekea huko Zanzibar kwa ajili kuiangalia timu hiyo iliyoanza na Mafunzo na kesho (jana) asubuhi atarejea kuendelea kukinoa kikosi chake.

“Kabla ya kocha (Papic) kuwaondoa wachezaji tisa kwenye timu A na kuwaunganisha kwenye timu ya U-20, waliokwenda kwenye Mapinduzi, alipanga kukibakisha kikosi kizima jijini Dar es Salaam.

“Baada ya mvutano wa muda mrefu kati yake na uongozi, ndipo akachukua uamuzi wa kuwaondoa Gumbo, Atiff na Kiiza ambaye hata hivyo ameshindwa kwenda Zanzibar baada ya kuchelewa kuwasili nchini, akitokea Uganda kumuuguza mama yake mzazi.

“Awali Papic aligoma kabisa kuipeleka timu Zanzibar, lakini baadaye alikubali na kuwaachia wachezaji hao tisa ambao alisema hawapo kwenye programu yake ya maandalizi ya michuano ya kimataifa na ligi,” kilisema chanzo hicho.

Wachezaji waliobaki na Papic Dar es Salaam ni Yaw Berko, Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Abuu Ubwa, Stephano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Chacha Marwa, Bakari Mbegu, Juma Seif ‘Kijiko’ na Godfrey Bonny.

Wengine ni Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima ‘Niyo’, Kigi Makasi, Shamte Ally, Kenneth Asamoah, Davies Mwape (ataungana na timu baada ya kutoka Zambia), Pius Kisambale, Omega Seme na Jerry Tegete.

Khatimu Naheka na Wilbert Molandi, GPL

No comments:

Post a Comment