Friday, January 6, 2012

Benni McCarthy azikosa Simba, Yanga


WAKATI mipango ya kuileta nchini timu yenye mashabiki wengi zaidi Afrika Kusini, Orlando Pirates ikiwa katika hatua za mwisho, mashabiki watakosa bahati ya kumuona mshambuliaji mtukutu wa timu hiyo, Benedict McCarthy.

Iwapo Orlando Pirates itakubali kuja nchini kucheza mechi za kirafiki dhidi ya Yanga na Simba, wakati huo McCarthy atakuwa akifanya kazi za kituo maarufu kinachorusha michezo barani Afrika, Super Sport.

Alexandre Bazzerra, ambaye yuko kwenye benchi la ufundi la Orlando, ameliambia Championi jijini hapa kuwa kama suala la kucheza Tanzania litafikia mwafaka, wana uhakika McCarthy hatakuwa nao.
“Benni alishatoa taarifa mapema, unajua kwa sasa PSL (Ligi Kuu ya Soka Afrika Kusini), imesimama hadi Kombe la Mataifa Afrika lipite. Hivyo uongozi ukampa ruhusa, maana yake hata tukicheza mechi ya kirafiki atakuwa hayupo kwenye programu,” alisema Bazzerra.

McCarthy, ambaye ni mshambuliaji kutoka Afrika Kusini mwenye mafanikio zaidi barani Ulaya, wakati huo atakuwa akifanya kazi ya uchambuzi kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kupitia Super Sport. Super Sport imewateua wachezaji nyota wa zamani na watangazaji kutoa tathmini kwenye michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Januari 21, mwaka huu katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea.

Pamoja na McCarthy wengine walioteuliwa ni Sammy Kuffour, Neil Tovey, Stephen Keshi, Daniel Amokachi, Doctor Khumalo, Shaun Bartlett na Gavin Hunt.

Kabla ya kurejea kucheza kwao, McCarthy alionyesha uwezo akiwa na timu mbalimbali za Ulaya kama Ajax (Uholanzi), Celta Vigo (Hispania), FC Porto (Ureno), West Ham United na Blackburn Rovers (England).

Na Saleh Ally, aliyekuwa Johannesburg - GPL

No comments:

Post a Comment