Wednesday, December 21, 2011

Maftah awekwa chini ya uangalizi


BEKI wa pembeni, Amir Maftah (pichani), atalazimika kuwa nje ya kikosi cha Simba kwa wiki moja zaidi ili apate nafasi ya kupona vizuri.

Maftah amekuwa nje ya uwanja tangu Septemba 18, mwaka huu alipoumia wakati wa mchezo dhidi ya Kagera Sugar na ingawa ameshapata nafuu, daktari wake, Cosmas Kapinga, amemwambia asijiunge na kikosi cha Simba kwa sasa.

Akizungumza na Championi Jumatano, Kapinga alisema beki huyo bado hajapona vizuri, hivyo, amemuandalia programu maalumu itakayomwezesha kurejea katika uimara wake.
“Atafanya mazoezi binafsi kwa wiki moja kabla ya kujiunga na wenzake katika mazoezi ya pamoja chini ya Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic ‘Profesa Chico’.

“Yatakuwa ni mazoezi binafsi mepesi kwa ajili ya kuimarisha kifundo chake,” alisema Kapinga.
Simba inaendelea na mazoezi makali. Asubuhi inafanya mazoezi ya ‘gym’ na jioni kwenye ufukwe wa Coco, Dar es Salaam, kwa ajili ya kujiwinda na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.


Na Wilbert Molandi, GlobalPublishers

No comments:

Post a Comment