Saturday, November 12, 2011

TAIFA STARS YAILAZA CHAD 2-1


KOCHA wa Taifa Stars, Jan Poulsen amepata ushindi wake wa kwanza ugenini tangu alipochukua timu hiyo kutoka kwa Mbrazil Marcio Maximo, Agosti mwaka jana baada ya leo kuifunga Chad mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya mchujo ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini Brazil.

Ikicheza kwa mara ya kwanza nchini Chad, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufunga dakika ya kumi katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya hapa N'Djamena kupitia kwa winga Mrisho Ngasa.

Hata hivyo, mashabiki wa Chad walisubiri kwa dakika tano tu kabla ya kusherehekea bao baada ya kiungo Mahamat Labo kuisawazishia dakika ya 15. Labo anachezea klabu ya Laval ya Ufaransa alitumia vizuri makosa ya mabeki wa Tanzania waliochelewa kucheza mpira wa krosi.

Dakika kumi kabla ya mwamuzi Bunmi Ogunkolade kutoka Nigeria hajapuliza filimbi ya kuhitimisha pambano hilo lililohudhuriwa na takribani mashabiki 10,000, Nurdin Bakari aliyeingia badala ya Abdi Kassim aliifungia Stars bao la pili.

Mpira ulianzia kwa mshambuliaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Thomas Ulimwengu ambaye akiwa wingi ya kulia alifanikiwa kumtoka beki wa kushoto wa Chad kabla ya kutumbukiza krosi iliyomkuta mfungaji.

Stars na Chad zinakutana tena Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya marudiano ambayo matokeo yake ndiyo yataamua timu ipi kati ya hizo itakayoingia hatua ya makundi,kwenye kundi ambalo lina timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.

Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Idrisa Rajab, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Shabani Nditi, Nizar Khalfan/Thomas Ulimwengu, Henry Joseph, Mbwana Samata/Mohamed Rajab, Abdi Kassim/Nurdin Bakari na Mrisho Ngassa.

Boniface Wambura Media Officer Tanzania Football Federation (TFF) +23592159563 N'Djamena

No comments:

Post a Comment