Saturday, November 12, 2011

Afya ya VENGU ni majonzi, vilio


AFYA ya staa wa Orijino Komedi ‘OK’, Joseph Shamba ‘Vengu’ (pichani) aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na ugonjwa unaodaiwa kushambulia sehemu ya kichwa, imeibua majonzi na vilio kwa mashabiki wake, wadau wa sanaa na
Watanzania kwa jumla.

Baada ya gazeti pacha na hili, Ijumaa Wikienda Jumatatu wiki hii kuripoti habari ya Vengu kukaa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa takribani miezi miwili, Ijumaa lilipokea simu na meseji nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakipeleka vilio vyao kwa wadau wa sanaa na serikali kuwa ufanyike utaratibu wa staa huyo kupelekwa India kwa ajili ya matibabu kama ilivyo kwa wanasiasa.

“Ukweli habari ya afya ya Vengu inaumiza sana. Nani asiyejua mchango wa Vengu? Hapa inahitajika nguvu ya pamoja ya hali na mali ili akatibiwe nje, apone na aendelee na harakati za kuitumikia jamii kwa vichekesho vyake vilivyojaa mafunzo,” zilisomeka baadhi ya meseji za wasomaji wa habari hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alikwenda kumjulia hali Vengu ambaye alikuwa ametolewa ICU na kuwekwa wodi namba moja katika Jengo la Mwaisela alipolazwa hadi sasa.

KUTOKA IJUMAA
Sisi sote ni ndugu, watoto wa baba mmoja. Vengu ni mwenzetu tena ni mfano wa kuigwa na vijana watafutaji. Mwenzetu anahitaji sala na dua zetu. Tunaamini wadau wa sanaa na serikali yetu sikivu watafanya jitihada za kumsaidia.

Na Sifael Paul, GlobalPublishersTz

No comments:

Post a Comment