Tuesday, October 18, 2011

NI kama msemo wa kutesa kwa zamu, kwani baada ya utawala wa watumishi kadhaa wa kiroho, sasa upepo umegeuka kwa Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Nabii Flora Peter.

Nabii Flora ambaye kanisa lake lipo Mbezi Beach, Dar es Salaam, anatajwa kuwa malkia wa miujiza kutokana na neno lake pamoja na mafuta anayotumia kuponya watu wenye maradhi na matatizo mbalimbali.

Uwazi limeelezwa kuwa watu wengi wanamiminika kwa Nabii Flora kupata tiba kwa sababu hutumia mafuta aliyoyaombea ambayo akimrushia muumini wake, hupona maradhi, mikosi na matatizo yote yenye mkono wa Shetani.

Waandishi wa gazeti hili wamefuatilia maombezi yanayofanywa na nabii huyo kwa wiki mbili sasa, waligundua kuwa mafuta yanayotumika ni ya mzaituni kutoka Israel na Nabii Flora huyaweka kwenye kisahani kabla ya kuanza kuwapaka au kuwamwagia watu wenye matatizo.

HUPONYA UKIMWI, UTASA, KISUKARI
Baadhi ya watu waliodai kuwa na maambukizi ya ukimwi walipanda juu ya madhabahu kanisani hapo na kusema kuwa wamepona, hali iliyofanya waumini wengine kushangilia.

Mmoja wa watu hao ni Mosi Suleiman, Mkazi wa Ukonga Majumbasita, alitoa ushuhuda kuwa alikuwa na ugonjwa huo tangu 2006 lakini Mei 5, mwaka huu alijiunga katika kanisa hilo na kushuhudia mbele ya umati wiki iliyopita kuwa amepona.

Aidha, mwanamke mmoja, Ruth Ezekiel ambaye alidai alikuwa na matatizo ya kizazi kwa muda mrefu na kuondolewa katika Hospitali ya Dar Group alisema baada ya kuombewa na nabii huyo, sasa ni mjamzito na anashangazwa na hilo.

Mwingine ambaye alitoa ushuhuda ni mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Tatu Mohamed, mkazi wa Magomeni Mapipa, Dar aliyedai kuwa alikuwa na ujauzito kwa miaka mitatu lakini baada ya maombezi ya mama huyo na kupakwa mafuta, alijifungua salama.

Naye Suleiman Mohammed aliyedai kuwa alikuwa na uvimbe kwenye mgongo kwa miaka 26, lakini baada ya kuombewa umetoweka na kuanzia siku hiyo ameamua kusali hapo.

“Siyo uvimbe tu bali pia nilikuwa na kipanda uso, baada ya maombezi nimepona kabisa,” alisema Mohammed.

Aidha, Frida John alidai mbele ya waumini kanisani hapo kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kisukari lakini baada ya maombezi tatizo hilo halipo tena, hivyo anamshukuru Mungu.
Na Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’


No comments:

Post a Comment