Wednesday, October 26, 2011



Na Haruni Sanchawa
UNAWEZA usiamini kuwa kuna kijana mzima kabisa aliamua kuchukua panga na kuicharanga familia nzima ya mjomba wake aliyemlea na kumsomesha kisha kumuua eti kwa kuwa alimkuta akisikiliza Kurani na yeye alitaka kusikiliza matangazo ya mpira!

Lakini ndivyo ilivyokuwa kwani mauaji ya kutisha yametokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo kijana mmoja, Abuu Bashir, anatuhumiwa kufanya unyama huo kwa familia hiyo ya mjomba wake aitwaye Mwalami Musa (55) na baadaye ametokomea porini.

Aliyeuawa kwa kukatwa na mapanga ametajwa kuwa ni mjomba mtu, Musa, Mkazi wa Kijiji cha Madafu, Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Habari kutoka katika eneo la tukio zinadai kuwa chanzo cha mauaji hayo kilikuwa kugombania redio ambapo marehemu Musa alikuwa anasikiliza Korani lakini kijana Bashir alitaka kusikiliza matangazo ya mpira.

Chanzo chetu cha habari kilisema hali hiyo inadaiwa ilisababisha kijana huyo Bashir kuingia ndani na kuchukuwa panga na kisu, alipotoka akaanza kucharanga watu ambapo marehemu alikatwa kichwani na sehemu nyingine mwilini na kusababisha atokwe na damu nyingi na hatimaye kufariki dunia akiwa anakimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Mwandishi wa gazeti alifika katika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya watu ambao walikiri kuwa chanzo cha kuuawa kwa panga marehemu na mpwa wake na kukatwa mapanga watoto wake ni ugomvi wa kugombea redio.

“Huyu kijana aliyeua kalelewa na marehemu ambaye ni mjomba wake, kitendo alichokifanya Bashir kimetushangaza sana,” alisema jirani mmoja ambaye hakuta jina lake liandikwe gazetini.

Aidha, katika vurugu hizo watoto watatu wa marehemu walijeruhiwa vibaya kwa kisu na kijana huyo, wametambulika kuwa ni Rajabu Mwalami (8), Shabani Mwalami (6) na Abuu Kiuta (5), wote walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kutibiwa.

Hata hivyo, hali ya watoto hao hazikuwa nzuri ambapo Abuu alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Uwazi lilifika katika hiyo na kukutana na muuguzi mkuu, Rosemary Magombala ambaye alisema majeruhi hao waliletwa hapo Oktoba 19, mwaka huu saa 2.45 usiku wakiwa katika hali mbaya.

Mke wa marehemu, Tatu Musa akisimulia tukio hilo alisema wakati vurugu zinatokea alikuwa jikoni.
“Nilishitukia watoto wakilia na nilipotoka jikoni nikamuona mume wangu amejiinamia damu zikimtoka, kumbe alikuwa tayari amekatwa panga, alichukuliwa na majirani kukimbizwa hospitali na akafia njiani,” alisema Tatu kwa majonzi.

Aidha, gazeti hili lilifika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuzungumza na muuguzi wa wodi namba 4 ya watoto, Ruth Ngaka ambaye alisema kuwa mtoto Abuu aliyeletwa hapo Oktoba 20, mwaka huu akiwa na hali mbaya lakini hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa operesheni.

Tayari tukio hilo limeripotiwa polisi Mkuranga na mtuhumiwa anasakwa ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

CHANZO: GPL

No comments:

Post a Comment