Thursday, October 20, 2011

MALKIA wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando (pichani) anasakwa kwa udi na uvumba ili auwawe. Hivi karibuni alivamiwa nyumbani kwake Ipagala, Dodoma na kundi la watu wasiojulikana ambao walimpiga picha kisha wakakimbia.

Habari zisizokuwa na chembe ya chenga zilizotua kwenye dawati la Amani juzikati zinasema kuwa kundi hilo lilifika nyumbani kwa Rose saa 12:30 jioni. Lilipofika liliwakuta vijana wake wakifanya mazoezi ya nyimbo na kuanza kupiga picha bila ridhaa yao, walipowashtukia wakakimbia.

“Kuna mpango umeandaliwa na baadhi ya watu wa kutaka kumuua Rose kihuduma na kiroho, na hivi karibuni alivamiwa na watu asiowajua wakati vijana wake wakifanya mazoezi ya nyimbo za albamu yake ya tatu ya ‘Nimeona Utamu wa Yesu’ anayotarajia kuirekodi katika mfumo wa video,” alisema mtoa habari wetu.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Rose alikiri kuvamiwa na kundi hilo na alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa kuna mwimbaji mmoja wa Injili ndiye anayefanya mchezo huo mchafu. Baada ya tukio hilo alisali sala ya mwisho kwa kufunga mazoezi hayo mpaka kesho yake.

“Ni kweli nilivamiwa na kundi hilo ambalo nahisi linatumiwa na mwimbaji mwenzangu wa Injili ambaye amekuwa akifanya kila njia kutaka kuniangamiza, lakini hawezi kwa sababu Mungu wangu atanipigania,” alisema Rose.

Rose aliendelea kusema kuwa mwimbaji huyo amekuwa akimuonea wivu kwa muda mrefu anapofanya huduma kwa mafanikio makubwa na kila anapotoa albamu mpya. Akaona njia sahihi ya kumzimisha ni kumpoteza kimwili na kiroho.

“Huduma hii nimepewa na Mungu, sikupewa na mwanadamu ndiyo maana naifanya kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu. Namuomba mwimbaji huyo kunyenyekea mbele ya Mungu ili ampake mafuta ya utumishi na atumike katika viwango vya juu,” alisema Rose.


Na Imelda Mtema, Global Publishers Tz

No comments:

Post a Comment