Thursday, July 28, 2011

WABUNGE CCM WAICHACHAFYA SERIKALI KWA VIFUNGU

Hali juzi na jana ilichafuka bungeni baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa kauli zinazoonyesha jinsi wasivyoridhishwa na utendaji wa Serikali inayoongozwa na chama chao.

Walitoa kauli hizo walipokuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe.

Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango–Malecela, yeye alitumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuichambua Serikali akinukuu toleo la mwaka 1977 sehemu ya pili ibara ya 8 (c) na 9 (i) ambayo inaeleza jinsi Serikali itakavyotumia rasilimali za nchi kuwaondolea umasikini Watanzania.
“Bei ya mazao ili imnufaishe mkulima lazima izidi gharama za uzalishaji, inapotokea gharama zinakuwa juu kuliko bei ya kuuzia, hapo mkulima anakuwa hafaidiki kwa namna yoyote.

“Katika mazungumzo yangu haya nitaitumia Katiba ya nchi yetu toleo la 1977, sehemu ya pili, ibara ya 8 (c) na 9 (i) ili wenyewe muone jinsi Serikali isivyowajali wakulima.

“Katika eneo hilo la Katiba, Serikali itatakiwa kuwaodolea Watanzania umasikini, sasa kwa mtindo huu kweli mnawaondolea umasikini? Hamuwezi kuzuia chakula kisiuzwe popote wakati nyinyi hamna uwezo wa kukinunua, hii haiwezekani.

“Katika gazeti moja linalotoka kila siku Waziri umenukuliwa ukisema nchi jirani zenye njaa zinatakiwa kuwasiliana na Serikali yetu ili ziuziwe chakula badala ya kupitia moja kwa moja kwa wakulima.

“Sasa Mheshimiwa Waziri, nakuuliza ni lini Serikali imeanza biashara ya kuuza chakula nje? Mnawakaribisha watu wa nje waje kununua chakula, hicho chakula mmekilima nyinyi? Nasema hili nalikataa, kwa nini mnauza chakula nje halafu wananchi mnawazuia?

“Waziri Mkuu nasema hapana, waacheni wakulima nao wanunue ma-VX, nitakuwa mtu wa ajabu kama nitasema naunga mkono jambo ambalo silipendi, siungi mkono hoja,” alisema Kilango.

Mbunge huyo alizungumzia pia Kiwanda cha Tangawizi kilichoko Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro na kuishutumu Serikali kwa kushindwa kuweka miundombinu ya maji na barabara kiwandani hapo ili wananchi weweze kunufaika na kiwanda hicho pindi kitakapoanza.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, mnataka niunge mkono hoja hii? Nasema sitaki japokuwa nakushukuru kwa kunipa Sh milioni 10, kiwanda kimeanzishwa tena ni kizuri kweli kweli, Serikali mkiombwa msaada hamtaki, kwa nini mko hivyo?” Alihoji.

...mengineyo, soma gazeti MTANZANIA

source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/07/wabunge-ccm-waichachafya-serikali-kwa-vifungu.html#ixzz1TOKL6GLo

No comments:

Post a Comment