Friday, July 8, 2011


ALIYEKUWA mkatanyonga namba moja wa Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Aisha Mohamed Mbengu ‘Aisha Madinda’ (pichani), ametoweka nyumbani kwa bosi wake Asha Baraka Magomeni Usalama, jijini Dar es Salaam alipokuwa akiuguzwa ugonjwa wa kuvimba miguu, Amani limebeba kabrasha la habari hii.

Kwa mujibu wa chanzo makini cha habari hizi, Aisha Madinda alitoweka Julai 4, mwaka huu baada ya kukumbwa na tuhuma za kupokea madawa ya kulevya kutoka kwa jamaa mmoja aitwaye Chande Mohamed.

Chande aling’ang’aniwa na walinzi wa bosi huyo nyumbani hapo kwa madai ya kumpelekea madawa hayo Aisha kwa ajili ya matumizi na alifikishwa katika Kituo cha Polisi Magomeni jijini Dar.

Siku moja baada ya kukamatwa kwa Chande, Aisha ‘alimtaimu’ bosi wakati akienda kwenye shughuli zake na kutokomea kusikojulikana.

Inadaiwa kuwa Aisha ambaye ni mnenguaji wa siku nyingi nchini, alikumbwa na wasiwasi mkubwa baada ya kukamatwa kwa Chande na kusemwa na Asha Baraka kuhusiana na kutoijali afya yake.

Chande ambaye amefunguliwa jalada la mashtaka namba RB/MAG/11342/2011, alikiri kumpelekea Aisha ‘unga’ mara kwa mara na kuongeza kuwa unga huo alikuwa akiagizwa na bosi wake aliyemtaja kwa jina la Ibrahim Lipumba mkazi wa Kinondoni Stereo jijini Dar.

Akilizungumzia tukio hilo, Asha Baraka alisema kwamba kwa upande wake amejivua gamba rasmi kumsaidia mnenguaji huyo ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kuvimba miguu.

Aisha Baraka alisema kuwa amehangaika kumtibia Aisha kwa hali na mali kwa muda wa miezi mitano na kutumia gharama kubwa lakini mgonjwa wake hakuwa akijionea huruma.
“Nilijitahidi kupigania afya yake ili aondokane na vishawishi vya kutumia madawa ya kulevya kwa kuishi naye nyumbani kwangu nikiamini kuwa angeweza kuachana nayo lakini imekuwa ni kazi bure,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa Twanga Pepeta alisema kuwa ameamua kubwaga manyanga na kama kuna mtu atamuona ni mbaya yuko tayari kukubali lawama hizo lakini wema wake kwa Aisha umeishia kwa kupoteza fedha zake nyingi bila ya mafanikio.

“Hata kwenye bendi yangu simuhitaji tena na sitashirikiana naye kwa jambo lolote, kuanzia sasa aendelee na mambo yake binafsi,”alisema Asha kwa uchungu.

Asha Baraka aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni na kufungua jalada la mashtaka namba RB/ MAG/11342/2011 baada ya jitahada za kumtafuta Aisha Madinda sehemu kadhaa kutozaa mafanikio.


CHANZO: GPL
http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/aisha-madinda-atoweka

No comments:

Post a Comment