Wednesday, June 29, 2011

Watuhumiwa wa ubadhirifu wa ardhi Manispaa ya Kinondoni wapanda kizimbani

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania, TAKUKURU, imewapandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni watendaji wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka 45 tofauti yakiwemo kutumia madaraka vibaya pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Watuhumiwa saba kati ya nane ndiyo walifika mahakamani hapo huku Patrick Makoyola akikosekana, ambapo mahakama iliamuru atafutwe na polisi na kufikishwa mahakamani hapo.

Waliosomewa mashataka mahakamani ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Ardhi Manispaa ya Kinondoni, Hamidu Mgaya; Ofisa Mtendaji Kilongawima Mbezi, Wanura Maranda; Mwenyekiti wa mtaa Kilongawima Mbezi, Francis Woiso na Diwani wa kata ya Kunduchi, Patrick Makoyola.

Wanne hao kwa pamoja walisomewa mashtaka na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Leonard Swai, aliyeieleza mahakama mbele ya Hakimu Yohana Yongolo kuwa watuhumiwa wamevunja kifungu namba 31 cha kuzuia na kupambana na rushwa kwa kutumia madaraka vibaya pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa waajiri wao ambapo, mwezi Juni na Julai 2008, watendaji hao walitoa taarifa za uongo kwa mkurugenzi wao zikionyesha kuwa eneo ambalo lililopo katika michoro ya mipango miji namba TR.DRG. 1/12/8001 kuwa linamilikiwa na Athumani Mahimbo ambapo walimsajili kwa namba ya eneo 2466 Block L Mbezi.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni Anna Macha (Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi); Mapambano Baseka (Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni); Said Waligwah (Ofisa Mtafiti wa ardhi Manispaa ya Kinondoni) na Hamidu Mgaya (Ofisa ardhi manispaa ya Kinondoni).

Wanne hao wanatuhumiwa kuitumia madaraka vibaya na kuvunja kifungu cha sheria namba 12(1) cha mwaka 1999 namba nne katika sheria ya michoro ya mipango miji kwa kummilikisha Kheri Mabira eneo walilolisajili kwa namba 2473 lililoko Block L Mbezi, eneo ambalo ni la wazi lililotengwa na Serikali kwa matumizi ya umma.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na walipata dhamana baada ya wadhamini kutimiza masharti waliosomewa na hakimu. Kesi itasomwa tena Julai 26, 2011.


source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/06/watuhumiwa-wa-ubadhirifu-wa-ardhi-manispaa-ya-kinondoni-wapanda-kizimbani.html#ixzz1QeIwIbNK

No comments:

Post a Comment