Wednesday, June 15, 2011

SIKU YA MTOTO WA AFRIKA


UTANGULIZI:
Mwaka 1990, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ulipitisha Azimio la nchi 51 za wanachama wa Umoja huo kuhusu kukumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto kilichopo Afrika ya Kusini ambao waliuawa kinyama na iliyokuwa Serikali ya Makaburu ya nchi hiyo tarehe 16 Juni, 1976.

Watoto hao walikuwa wakidai haki ya kutobaguliwa na haki nyingine za kibinadamu.

MADHUMUNI:
Pamoja na kukumbuka mauaji hayo ya kinyama, madhumuni mengine ya kuadhimisha siku hiyo ni pamoja na yafuatayo: kuwa na fursa ya kusisitiza wajibu wa Serikali za Afrika kwa watoto; kuziwezesha Serikali hizo kuandaa na kutekeleza mipango ya taifa ya kuwaendeleza watoto; Kuinua kiwango cha uelewa na ufahamu wa matatizo yanayowakabili watoto wa Afrika.

Tanzania ikiwa ni nchi mojawapo mwanachama wa Umoja wa Afrika, imekuwa ikishiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku hii kwa miaka kumi na saba (17) mfululizo tangu mwaka 1991. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania hutumia siku hii kutafakari kwa kina matatizo mbalimbali yanayowakabili watoto na vile vile kutafuta namna ya kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo.

Serikali inapata pia wakati mzuri wa kutangaza sera, programu na mipango mbalimbali inayohusu masuala ya watoto na kuhamasisha jamii kuchangia kuondoa matatizo mbalimbali ya watoto kote nchini.

Kwa upande mwingine, maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa sera zetu zinazohusu kuwaendeleza watoto, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu haki na ustawi wa watoto.

KAULI MBIU:
Kaulimbiu ya mwaka 2011 inasema “Tuungane kwa Pamoja Kuchukua Hatua za Haraka Kushughulikia Tatizo la Watoto Wanaoishi Mitaani (All Together for Urgent Actions in Favour of Street Children)”.

Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa kuna haja ya kuliangalia upya tatizo la ongezeko la watoto wanaoishi mitaani kutokana na hali halisi ya tatizo hili linavyoonekana hapa nchini..

SHUGHULI ZITAKAZOFANYIKA:
Maadhimisho haya huambatana na shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo hufanyika kitaifa na kimkoa. Mwaka huu hapatakuwepo na maadhimisho kitaifa, bali kila mkoa utapata fursa ya kupanga namna ya kuadhimisha siku hii kulingana na rasilimali zilizopo mkoani, wilayani na vijijini.

MWISHO:
Ni matarajio ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuwa vyombo vya habari vitatoa ushirikiano wa hali ya juu katika kuhamasisha jamii yetu juu ya umuhimu wa Siku hiyo.

Vile vile, Wizara inapenda kutumia fursa hii kuikumbusha mikoa kuhakikisha kuwa siku hiyo inaadhimishwa katika maeneo yao na kwa kutumia rasilimali walizo nazo.

Mwisho, ninapenda kuchukua tena fursa hii kuwakumbusha Watanzania wote na viongozi wetu hapa nchini kuwa watoto ni taifa la leo na la kesho, hivyo wanapaswa kuendelezwa, kulindwa, kushirikishwa, kuishi na kutokubaguliwa Nawatakia kila la kheri katika kufanikisha maadhimisho haya.

WATOTO NI TAIFA LA LEO NA KESHO.

Kijakazi.R. Mtengwa
KATIBU MKUU

source: http://www.wavuti.com/4/post/2011/06/siku-ya-mtoto-wa-afrika.html#ixzz1PKPGNSJF

No comments:

Post a Comment