Monday, June 27, 2011

MAONI YA WAZIRI SITTA KUHUSU POSHO YANAGUSA


Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechangia maoni yake kuhusu mjadala wa posho za wanasiasa na watendaji wengine akisema suala hilo linapaswa kuanzia katika ngazi ya chini.

Amesema wanataaluma ndio wanatakiwa kulipwa vizuri tena kwa fedha nzuri kuliko wanasiasa.

Alisema kuwa wanataaluma wangepaswa kulipwa zaidi kuliko wanasiasa kutokana na kuwa wamehangaikia taaluma zao kwa miaka mingi kuliko wanasiasa, akieleza kuwa siasa ni kitu cha kujitolea.

"Sioni sababu ya wabunge kuendelea kujadiliana na kubishana juu ya suala hili la posho... Kinachotakiwa ni kumlipa vizuri mtu aliyehangaikia taaluma yake tena kwa muda mrefu, inafaa apewe mshahara mzuri kulingana na taaluma yake, lakini kwa nchi yetu wataalamu wanalipwa mishahara midogo ambayo haikidhi hata mahitaji yao ya msingi... Matokeo yake, wengi wakishamaliza elimu yao wanakimbilia nje ya nchi kufanya kazi au kugeukia siasa,” alisema Sitta.

Waziri Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuambia mdahalo ulioandaliwa na Jumuia ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe juzi kujadili masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki, alisema kuwa fedha nyingi zimekuwa zikipotea na hata wananchi wanapojaribu kuhoji hakuna maelezo yanayotolewa kwao na baadhi ya watendaji wa Serikali zikiwamo za vijiji, “Inashangaza kuona fedha nyingi zinapotea kuanzia vijijini na watendaji wake wamekuwa wakijilipa na kufanyia mambo yao bila kushirikisha wananchi na hata kutowasomea mapato na matumizi ya kijiji husika bila ufuatiliaji na wala hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika,”alisema.

Alisema ndani ya Serikali ya Tanzania kuna tatizo la uwajibikaji na watumishi wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kujisahau kuwa wanatakiwa kuwahudumia wananchi katika masuala ya kimaendeleo.


- Lilian Lucas, Morogoro via gazeti Mwananchi

source: http://www.wavuti.com/4/category/all/1.html#ixzz1QTeE1IW3

No comments:

Post a Comment